REKODI YA DUNIA HAIKUVUNJWA

Madai kuwa mwanamke wa Afrika Kusini alijifungua watoto 10 sio ya kweli, uchunguzi umebaini

Mamlaka ya Afrika Kusini inasema kwamba Gosiame Sithole mama wa watoto 10 hakuwa na ujauzito.

Muhtasari

•Mamlaka ya mkoa wa Gauteng inasema kwamba wamefanya uchunguzi wa kina kubaini kwamba hakuna hospitali ya umma au ya kibinafsi ilioweka rekodi za kujifungua kwake.

•Kulingana na mwandishi wa BBC Vumani Mkhize , hatua hiyo inajiri baada ya mwanamke huyo kudaiwa kujifungua Watoto kumi madai ambayo hayakuthibitishwa.

•Michango ilianza kumiminika kwa wanandoa hao na watoto wao , waliopatiwa jina ''Thembisa 10'' , ikiwemo $70,000; £50,000 kutoka kwa mwenyekiti wa IOL Iqbal Survé.

Gosiame Sithole alipigwa picha mwezi Mei na chombo kimoja cha habari cha Pretoria
Gosiame Sithole alipigwa picha mwezi Mei na chombo kimoja cha habari cha Pretoria
Image: Hisani

Mamlaka ya Afrika Kusini inasema kwamba Gosiame Sithole mama wa watoto 10 hakuwa na ujauzito.

Mamlaka ya mkoa wa Gauteng inasema kwamba wamefanya uchunguzi wa kina kubaini kwamba hakuna hospitali ya umma au ya kibinafsi ilioweka rekodi za kujifungua kwake.

Kulingana na mwandishi wa BBC Vumani Mkhize , hatua hiyo inajiri baada ya mwanamke huyo kudaiwa kujifungua Watoto kumi madai ambayo hayakuthibitishwa.

Lakini hii leo mamlaka ya Gauteng imetamatisha sakati ya kisa hicho cha Watoto 10.

Katika taarifa , idara ya afya inasema kwamba Gosiame Sithole hakujifungua hivi karibuni , na wala hakuwa na ujauzito wowote.

Taarifa hiyo hatahivyo haikueleza sababu za bi Sithole kubuni taarifa hiyo , lakini maafisa wa afya wamesema kwamba anapokea usaidizi wa kisaikolojia na ule wa kijamii.

Mwandishi aliyechapisha habari hiyo Piet Rampedi amejipata mashakani - baada ya serikali kuagiza afisi ya mwanasheria mkuu kumfungulia mashtaka.

Bwana Rampedi aliandika msururu wa habari akidai kwamba bi Sithole alijifungua Watoto 10

.

Ujauzito huo ulivutia hisia tofauti katika mitandao ya kijamii kote duniani na watu wakaanza kutuma ufadhili kwa wazazi wa Watoto hao.

Hatahivyo habari hiyo ilivutia shauku baada ya bwana Rampedi kushindwa kutaja hospitali ambayo watoto hao walizaliwa ,huku baadhi ya hospitali katika mkoa huo zikipinga madai kwamba mama huyo alikuwa amejifungua katika hospitali zao.

Shirika la habari la Mitandaoni Independent Online IOL, ambalo linamiliki Pretoria News na ambalo ndilo la kwanza kuripoti habari hiyo lilisimama kidete na kuunga mkono taarifa yake.

Siku ya Jumanne, taarifa iliovuja ilisema kwamba bwana Rampedi aliomba msamaha katika chombo cha habari cha Independent , akisema kwamba hiyo ilikuwa habari nzuri na kwamba alihisi hakuna haja ya kuyafanyia uchunguzi madai ya bi Sithole.

Je habari hiyo ilitoka wapi ?

Bi Sithole, ambaye ana pacha wa miaka sita na mpenzi wake Teboho Tsotetsi aliishi Thembisa , mji mdogo ulio na wafanyakazi wengi katika mkoa wa Gauteng karibu na mji wa Johannesburg.

Kulingana na IOL, walikuwa wakienda katika kanisa moja na bwana Rampedi ambaye alijulishwa kuwahusu mwezi Disemba.

Mnamo mwezi Mei inadaiwa aliwahoji wanandoa hao ambao walidai kwamba walikuwa wakitarajia watoto wanane - picha iliopigwa ilimuonesha bi Sithole akiwa na mimba kubwa.

Kujifungua kwake kulitangazwa na vyombo vya habari mjini Pretoria tarehe nane mwezi Juni vikimnukuu bwana Tsotesti kama chanzo.

Baadaye alisema kwamba alipokea ujumbe wa simu kutoka kwa mpenzi wake akimuelezea kuhusu tukio hilo na kuongezea kwamba hakuruhusiwa kutoka katika hospitali hiyo kutokana na masharti ya corona .

Rampedi pia alitegemea ujumbe wa WhatsApp na hakuthibitisha kutoka kwa hospitali.

Rampedi pia alitegemea ujumbe wa mtandao wa WhatsApp na hakuthibitisha kutoka kwa hospitali iliotoa habari hiyo.

Meya wa eneo hilo baadaye alithibitisha kijifungua kwa mwanamke huyo - na ni wakati huo ndiposa vyombo vingine vya habari ikiwemo BBC , vilichapisha habari hiyo - lakini msemaji wa serikali baadaye alisema kwamba mwanasiasa huyo aliwanukuu Bi Sithole na mume wake na kwamba hakuna aliyewaona watoto hao.

Michango ilianza kumiminika kwa wanandoa hao na watoto wao , waliopatiwa jina ''Thembisa 10'' , ikiwemo $70,000; £50,000 kutoka kwa mwenyekiti wa IOL Iqbal Survé.

Lakini habari hiyo ilizua wasiwasi baada ya chombo cha habari cha Pretoria kushindwa kubaini hospitali ambayo watoto hao walizaliwa huku baadhi ya hospitali mkoani Gauteng zikijitenga na tukio hilo lisilo la kawaida.

Hatahivyo wanandoa hao walitofautiana baadaye huku bwana Tsotesti akiripoti kutoweka kwa bi Sithole na kuwawataka watu kutotuma michango yao wiki moja baadaye huku naye mwanamke huyo akisema kwamba bwana Tsotetsi alikuwa akitaka kujinufaisha kifedha kutoka kwa watoto hao, kilisema chombo cha habari cha Pretoria News.

Wakati huohuo wafanyikazi wa kijamii walifanikiwa kumpata bi Sithole na alilazwa hospitalini ili kufanyiwa vipimo Ijumaa iliopita , ilisema mamlaka ya Gauteng

Taarifa iliovuja na kupatikana na News 24 ilidai kwamba Rampedi ameomba msamaha kwa kuharibu sifa yake akisema kwamba angeifanyia uchunguzi wa kina habari hiyo kabla ya kuichapisha.

(Uhariri: Samuel Maina)