UBAKAJI WA NDOA

"Mume wangu alikuwa malaika-kisha akanibaka" Mwanamke asimulia alivyobakwa na mumewe

Usiku wa harusi yake, Safaa mwenye umri wa miaka 34 alibakwa na mumewe.

Muhtasari

•Usiku wa harusi yake, Safaa mwenye umri wa miaka 34 alibakwa na mumewe. Tukio hilo lilimwacha na majeraha kwenye kinena chake, mkononi na kwenye mdomo.

•Katika utafiti wake wa hivi karibuni, uliochapishwa mnamo Januari 2015, Baraza la Kitaifa la Wanawake (NCW) linaloongozwa na serikali limesema kuwa kila mwaka kulikuwa na visa zaidi ya 6,500 vya unyanyasaji katika ndoa na uliohusisha ubakaji wa ndoa, unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vya kulazimishwa kingono.

Image: GETTY IMAGES

Wanawake nchini Misri wameanza kuvunja kimya kuhusu unyanyasaji wa kijinsia. Sasa moja ya mapambano ya hivi karibuni ni dhidi ya ubakaji wa ndoa, suala ambalo hadi hivi karibuni limekuwa mwiko.

Onyo: Nakala hii ina maelezo ya unyanyasaji wa kingono

Usiku wa harusi yake, Safaa mwenye umri wa miaka 34 alibakwa na mumewe. Tukio hilo lilimwacha na majeraha kwenye kinena chake, mkononi na kwenye mdomo.

"Nilikuwa kwenye hedhi na sikuwa tayari kufanya mapenzi usiku huo," anasema. "Mume wangu alidhani nilikuwa nikikwepa kushiriki mapenzi naye. Alinipiga, akanifunga pingu, akaziba mdomo wangu na kunibaka."

Safaa, hata hivyo, alikataa kupiga ripoti kwa dhidi ya mumewe kwa kuhofia unyanyapaa wa kijamii. Utamaduni wa kuwalaumu wahasiriwa ni jambo la kawaida hapa katika jamii ya mfumo dume, haswa ikiwa aliyeathiriwa ni mwanamke.

Lakini mabadiliko yalikuja mnamo Aprili, wakati kipindi kimoja cha runinga kinachoitwa Newton's Cradle ambacho kilipeperushwa wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu Ramadhani

Image: GETTY IMAGES

Kwa wanawake wengi, kipindi hiki kiliibua kumbukumbu mbaya lakini pia kiliwapa ujasiri wa kwenda kwenye mitandao ya kijamii na kubadilishana visa vya masaibu yao.

Katika wiki chache, mamia ya ushuhuda ulionekana mitandaono, pamoja na zaidi ya 700 kwenye ukurasa wa Facebook uitwao Speak Up.

Miongoni mwa ushuhuda huo ulikuwepo wa Sanaa mwenye umri wa miaka 27.

"Alikuwa malaika. Mwaka mmoja baada ya ndoa yetu, nilikuwa mjamzito na nilikuwa karibu kujifungua," anasema katika ujumbe kwa ukurasa huo. "Tuligombana juu ya kitu kidogo na aliamua kuniadhibu.

"Alijilazimisha kwangu na kunibaka. Nikapoteza mimba."

Sanaa amekuwa katika vita peke yake kupata talaka na sasa wametengana na mumewe lakini anaendelea kuhuzunika kwa kumpoteza mtoto wake.

Ngono ya kulazimishwa imeenea katika maeneo mengi ya Misri, haswa usiku wa harusi.

Mjadala kuhusu suala hilo ulizidi kuwa mkali wakati mke wa zamani wa mwimbaji mashuhuri alipotumia Instagram kudai kwamba alipitia ubakaji wa ndoa. Akitokwa machozi, video yake ilienea na ikagonga vichwa vya habari.

Mume wake huyo wa zamani alikataa madai hayo kuwa "hayana msingi" kwenye video aliyochapisha kwenye Instagram .

Mkewe wa zamani alitaka mabadiliko katika mfumo wa sheria ili uhalifu huo uwe wa jinai.

Katika utafiti wake wa hivi karibuni, uliochapishwa mnamo Januari 2015, Baraza la Kitaifa la Wanawake (NCW) linaloongozwa na serikali limesema kuwa kila mwaka kulikuwa na visa zaidi ya 6,500 vya unyanyasaji katika ndoa na uliohusisha ubakaji wa ndoa, unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vya kulazimishwa kingono.

"Ubakaji wa ndoa unalaumiwa juu ya utamaduni wa kawaida hapa Misri ambao unaamini kuwa mkataba wa ndoa unamfunga mke kua tayari kwa tendo la ndoa 24/7," anasema Reda Danbouki, wakili na mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Wanawake cha Mwongozo na Uhamasishaji wa Sheria .

Imani ya kawaida hapa, kulingana na tafsiri zingine za kidini, ni kwamba ikiwa mwanamke anakataa kufanya ngono na mumewe, anakuwa "mwenye dhambi" na "malaika wanamlaani usiku kucha", anaongeza.

Ili kumaliza mjadala, Dar al-Ifta, shirika la ushauri la Waislam la Misri ambalo linatoa amri za kidini, limesema: "Ikiwa mume anatumia nguvu kulazimisha mkewe kulala naye, yeye ni mtenda dhambi na mke ana haki ya kwenda kortini na kufunga mashtaka dhidi yake ili aadhibiwe. "

Bado, Kituo cha Wanawake cha Mwongozo na Uhamasishaji wa Sheria kimesajili visa 200 vya ubakaji wa ndoa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, haswa kwa sababu ya kile kinachojulikana kama "hofu ya usiku wa kwanza", Bwana Danbouki anaelezea.

Sheria za Misri hazijapiga marufuku ubakaji wa ndoa - jambo ambalo linachukuliwa kuwa aina ya unyanyasaji wa kijinsia na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) - na mahakama pia inapata ugumu kuthibitisha.

Kesi nyingi za ubakaji wa ndoa ambazo huenda kortini haziishii kwa kupatikana hatiani kwa washukiwa kutokana na Kifungu cha 60 cha Sheria ya Adhabu ya Misri.

"Masharti ya Kanuni ya Adhabu hayatatumika kwa tendo lolote lililofanywa kwa nia njema, kulingana na haki iliyoamriwa kwa mujibu wa Sharia (sheria ya Kiislamu)," kifungu hicho kinasema.

Lakini Bw Danbouki anasema kuwa ubakaji wa ndoa unaweza kuthibitishwa kwa "kuchunguza mwili wote kutafuta majeraha ya nje. Vidonda karibu na mdomo vinapaswa kutafutwa, pamoja na mikono".

Mabadiliko mara nyingi huja polepole Misri, ambapo maadili ya kihafidhina bado yanatawala, lakini kwa wahanga wa ubakaji wa ndoa, sauti zao zinaanza kusikika.