logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Hospitali yachunguzwa baada ya mjamzito kutolewa figo bila kujitambua

Madaktari walieleza kuwa hiyo ndiyo njia pekee iliyokuwa ya kuokoa maisha yake.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri27 May 2022 - 10:15

Muhtasari


•Mjamzito huyo ameelezea jinsi alivyokimbizwa hospitalini akiwa katika hali mbaya na kuhitajika kufanyiwa upasuaji, lakini figo yake ikadaiwa kuvunwa.

•Msemaji wa polisi wa mkoa wa Wamala, Rachel Kawala, alisema wamechukua taarifa za mgonjwa na uchunguzi wa kisa hicho unaendelea.

Polisi wilayani Mubende nchini Uganda wanachunguza kuhusu madktari wasio waaminifu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa baada ya kudaiwa kutoa figo kutoka kwa mama mjamzito ambaye alikuwa hajitambui.

Mjamzito huyo Peragiya Muragijemana, 20, ni mkazi wa Kijiji cha Lwemiggo, wilayani Mubende anaelezea jinsi alivyokimbizwa hospitalini akiwa katika hali mbaya na kuhitajika kufanyiwa upasuaji, lakini figo yake ikadaiwa kuvunwa.

Bi Muragijemana anasema alijifungua mikononi mwa mkunga wa jadi, lakini alishindwa kutoa kondo la nyuma, na kusababisha kutokwa na damu nyingi.

“nilipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya Mubende, ambapo mume wangu, Amos Tiringanya, alitakiwa kusaini hati ya kuniruhusu kufanyiwa upasuaji,” alisema katika mahojiano na gazeti la Daily Monitor.

Mume wake alisema kuwa madaktari walimueleza kuwa ndiyo njia pekee ya kuokoa maisha yake kwani alikuwa akivuja damu.

“Baada ya upasuaji, mke wangu alirudishwa wodini akiwa amepoteza fahamu na aliruhusiwa baada ya siku tatu kutokana na msongamano hospitalini. Tulimpeleka nyumbani kwa mama mkwe wangu ,” alisema.

Aliongeza: “Lakini baada ya siku tatu, nilipigiwa simu na mama mkwe akinijulisha kuwa mke wangu amepata matatizo ya tumbo. Tulienda kwa uchunguzi wa hali ya juu zaidi, ambao ulionyesha kuwa figo yake ya kulia haikuwepo. Nilitia saini tu hati inayokubali kuondolewa kwa uterasi ya mke wangu ili kuokoa maisha yake, si figo yake.”

Mamake wa muathirika Piyera Musanabeera, alitoa taarifa kwa polisi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madaktari waliodaiwa kutoa figo ya binti yake.

Dkt Onesmus Kibaya, msimamizi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mubende, alishauri familia ya Muragijemana kuwa watulivu kwani hospitali hiyo pia inafanya uchunguzi wake.

Anaeleza kuwa mwanamke anapokuwa mjamzito, viungo vikuu hupata matatizo. Viungo hivyo ni pamoja na moyo, figo na uterasi.

"Mbali na hilo, hospitali ya Mubende haina uwezo wa kufanya upasuaji wa figo bali hufanywa katika hospitali ya Mulago".

Msemaji wa polisi wa mkoa wa Wamala, Rachel Kawala, alisema wamechukua taarifa za mgonjwa na uchunguzi wa kisa hicho unaendelea.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved