Rais wa Sri Lanka Gotabaya Rajapaksa ameikimbia nchi kwa ndege ya kijeshi, huku kukiwa na maandamano makubwa kuhusu mzozo wa kiuchumi.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73 aliwasili katika mji mkuu wa Maldives, mwendo wa saa 03:00 kwa saa za huko (22:00 GMT), BBC inachokifahamu.
Kuondoka kwa Bw Rajapaksa kunamaliza nasaba ya familia ambayo imetawala Sri Lanka kwa miongo kadhaa. Alikuwa amejificha baada ya umati wa watu kuvamia makazi yake siku ya Jumamosi.
Ndugu yake, Waziri wa zamani wa Fedha Basil Rajapaksa, pia ameondoka nchini, vyanzo vimeiambia BBC. Inasemekana anaelekea Marekani.
Wakati habari za kuondoka kwa rais zikiendelea, kelele zilizuka miongoni mwa waandamanaji katika eneo la Galle Face Green, eneo kuu la maandamano katika mji mkuu wa Colombo.
Siku ya Jumanne jioni tayari kulikuwa na maelfu ya watu wakikusanyika katika bustani hiyo, wakisubiri kujiuzulu kwa rais.
Raia wa Sri Lanka wanalaumu utawala wa Rais Rajapaksa kwa mzozo wao mbaya zaidi wa kiuchumi katika miongo kadhaa.
Kwa miezi kadhaa wamekuwa wakihangaika na kukatika kwa umeme kila siku na uhaba wa mambo ya msingi kama vile mafuta, chakula na dawa.
Kiongozi huyo ambaye ana kinga ya kutoshtakiwa wakati akiwa rais, inaaminika alitaka kukimbilia nje ya nchi kabla ya kuondoka madarakani ili kuepusha uwezekano wa kukamatwa na utawala mpya.
- Sri Lanka ni taifa la kisiwa kutoka kusini mwa India:
Lilipata uhuru kutoka kwa utawala wa Uingereza mwaka 1948. Makabila matatu - Sinhalese, Tamil na Muslim - hufanya 99% ya wakazi milioni 22 wa nchi hiyo.
- Familia moja ya ndugu imetawala kwa miaka mingi:
Mahinda Rajapaksa alikua shujaa kati ya Wasinhali walio wengi mwaka wa 2009 wakati serikali yake ilipowashinda waasi wanaotaka kujitenga wa Kitamil baada ya miaka mingi ya vita vikali na vya umwagaji damu vya wenyewe kwa wenyewe.
Kaka yake Gotabaya, ambaye alikuwa waziri wa ulinzi wakati huo, ndiye rais wa sasa lakini anasema anajiuzulu.
- Madaraka ya Urais:
Rais ni mkuu wa nchi, serikali na jeshi nchini Sri Lanka lakini anashiriki majukumu mengi ya kiutendaji na Waziri Mkuu, ambaye anaongoza chama tawala bungeni.
- Sasa msukosuko wa kiuchumi umesababisha ghadhabu mitaani:
Mfumuko wa bei umesababisha baadhi ya vyakula, dawa na mafuta kukosekana,kuna uhaba wa umeme na watu wa kawaida wameingia mitaani kwa hasira huku wengi wakilaumu familia ya Rajapaksa na serikali yao.
Ushindi mkubwa kwa waandamanaji
Ni anguko lilioje kwa Rais Gotabaya Rajapaksa - kwa muda mrefu kama mtu mkuu huko Sri Lanka.
Wachache walitarajia kwamba mambo yangeenda hivi.
Akiwa mkuu wa zamani wa ulinzi alisimamia oparesheni za kijeshi katika vita vyenye utata dhidi ya waasi wa Tamil Tiger vilivyomalizika mwaka wa 2009.
Anashutumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa vita na pia kuwalenga wale waliopinga, lakini amekuwa akikanusha shutuma hizo.
Familia ya Rajapaksa imetawala siasa za Sri Lanka kwa miongo miwili, na kwa kuungwa mkono na Wabuddha wengi wa Sinhala, alikua rais mnamo 2019.
Kuondoka kwake ni ushindi wa ajabu kwa waandamanaji waliofika barabarani kuelezea hasira zao dhidi ya usimamizi mbaya wa uchumi na kuongezeka kwa gharama ya maisha.
Kuondoka kwa rais kunatishia kuwepo kwa ombwe la mamlaka nchini Sri Lanka, ambalo linahitaji serikali inayofanya kazi kusaidia kuanza kuiondoa katika uharibifu wa kifedha.
Wanasiasa kutoka vyama vingine wamekuwa wakizungumza kuhusu kuunda serikali mpya ya umoja lakini hakuna dalili kwamba wako karibu kukubaliana.
Haijabainika pia kama umma utakubali kile wanachokuja nacho.
Chini ya katiba, ni Waziri Mkuu, Ranil Wickremesinghe, ambaye anafaa kuchukua nafasi ya rais iwapo rais huyo atajiuzulu.
Waziri mkuu anachukuliwa kuwa naibu wa rais bungeni.
Hata hivyo, Bw Wickremesinghe pia hapendwi sana.
Waandamanaji walichoma moto makazi yake ya binafsi siku ya Jumamosi - yeye na familia yake hawakuwa ndani - na alisema atajiuzulu ili kutoa nafasi kwa serikali ya umoja, lakini hakutoa tarehe.
Hilo linamwacha spika wa bunge kama ndiye anayetarajiwa zaidi kuchukua nafasi kama rais wa mpito, wataalamu wa katiba wanasema.
Lakini Mahinda Yapa Abeywardena ni mshirika wa Rajapaksas, na haijulikani kama umma utakubali mamlaka yake.
Yeyote atakayekuwa kaimu rais ana siku 30 za kufanya uchaguzi wa rais mpya kutoka miongoni mwa wabunge. Mshindi wa kura hiyo basi ataweza kumalizia muda uliosalia wa Bw Rajapaksa hadi mwishoni mwa 2024.
Siku ya Jumatatu, kiongozi mkuu wa upinzani Sajith Premadasa aliiambia BBC kuwa atawania kiti cha urais.
Lakini pia anakosa kuungwa mkono na umma na kuna mashaka makubwa ya umma kwa wanasiasa kwa ujumla.
Vuguvugu la maandamano ambalo limeifikisha Sri Lanka kwenye ukingo wa mabadiliko pia halina mpinzani dhahiri wa uongozi wa nchi hiyo.