Katika mkutano wa kwanza uliowaleta pamoja mawaziri wa mambo ya nje wa DR Congo na Rwanda, viongozi hao wamekubaliana kuhusu makubaliano ya amani "kati ya pande zinazozozana mashariki mwa DRC" ambayo yataanza kutekeleza Jumapili tarehe 04 mwezi ujao wa Agosti.
Ni uamuzi uliotolewa katika kikao kilichofanyika Luanda, Angola Jumanne kati ya Thérèse Kayikwamba Wagner upande wa Kongo na Olivier Nduhungirehe wa Rwanda, akiungana na mwenzao Tete Antonio wa Angola.
Katika matangazo yaliyochapishwa na wizara za pande zote mbili, Rwanda na DRC, walisema kuwa tukio hilo litadhibitiwa na chombo cha pamoja cha ufuatiliaji wa masuala ya usalama kati ya Rwanda na Congo.
Rwanda inasema kuwa "bado inaendelea kuwa na nia ya kufikia amani ya kudumu katika eneo hilo kwa kutatua vyanzo vya mzozo huu".
Congo inaishutumu Rwanda kwa kuwasaidia wapiganaji wa M23, na Rais Félix Tshisekedi aliendelea kusema kwamba hatazungumza na M23, akisema kwamba Rwanda iko nyuma yake. Rwanda inakana shutuma hizo