Watu kadhaa wameuawa kwa kupigwa risasi nchini Nigeria katika mji wa Kano, kaskazini mwa Nigeria wakati wa maandamano ya kulalamikia gharama ya juu ya maisha.Baadhi ya waandamanaji walijeruhiwa, na kupelekwa hospitalini.
Walioshuhudia walisema kuwa risasi zilipatikana kwenye eneo la tukio.Serikali haijatoa tamko lolote. Katika mji mkuu, Abuja, vikosi vya usalama vilitumia gesi ya kutoa machozi na kufyatua risasi hewani kujaribu kuwatawanya watu hao.
Mikutano ya hadhara imekuwa ikifanyika katika miji mikubwa nchini kote na vijana wa Nigeria wakiitaka serikali kushughulikia matatizo ya kiuchumi na kurejesha ruzuku ya mafuta ambayo ilitupiliwa mbali mwaka jana.
Amri ya kutotoka nje imewekwa katika jimbo la pili kwa ukubwa nchini Nigeria, Kano, baada ya maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha.
Kano ilishuhudia umati mkubwa zaidi katika siku ya kwanza ya maandamano ya kitaifa ambayo yalilazimu biashara nyingi kufungwa.
Waandamanaji katika majiji yote makubwa waliingia barabarani, wakiimba kauli mbiu kama vile: “Tuna njaa.”