Kile ambacho ulimwengu wote umeona kama kashfa ya video za ngono inaweza kuwa sehemu ya hiki kilichoshuhudiwa hivi karibuni katika maisha halisi kuhusu nani atakuwa rais ajaye wa Equatorial Guinea.
Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, mamia ya video za ngono zinazomhusisha mtumishi wa serikali wa ngazi ya juu wa Equatorial Guinea, pamoja na wanawake tofauti zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Video hizo zilifurika kwenye mitandao ya kijamii, na kuwashtua
watu katika nchi hiyo ndogo ya Afrika ya kati na kwingineko.
Wanawake wengi waliorekodiwa walikuwa wake na jamaa za watu walio karibu nae na maafisa mashuhuri ofisini kwake katika wizara ya fedha.
Baadhi wanaonekana walikuwa wanajua kuwa wanarekodiwa wakati wakifanya ngono na Baltasar Ebang Engonga, ambaye pia anajulikana kama "Bello" kutokana na ‘’muonekano wake mzuri’’
Hata hivyo Haya yote ni vigumu kuthibitisha kwani Equatorial Guinea ni taifa lenye sheria kali ambapo hakuna uhuru wa vyombo vya habari.
Hata hivyo kumekuwa na mtazamo kwamba uvujaji huo wa video za ngono ulikuwa mbinu ya kumdhoofisha ama kumuaibisha mtu aliye katikati ya dhoruba.
Bwana Engonga ni mpwa wa Rais Teodoro Obiang Nguema na mmoja wa wale wanaodhaniwa kuwa wanatarajia kurithi nafasi yake.
Obiang ndiye rais aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi kuwahi kutawala tangu 1979.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 82 amesimamia ukuaji wa uchumi ambao umegeuka na kudhoofu kutokana na akiba ya mafuta ambayo sasa inatajwa kupungua.
Kuna idadi ndogo ya wasomi na matajiri, lakini idadi kubwa ya raia milioni 1.7 nchini humo wanakabiliwa na umaskini.
Utawala wa Obiang unakosolewa vikali kwa rekodi yake ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kiholela na utesaji, kulingana na ripoti ya Marekani.
Pia umekumbwa na kashfa - ikiwa ni pamoja na kufichuliwa kwa maisha ya anasa ya mmoja wa watoto wa kiume wa rais, ambaye sasa ni makamu wa rais ambaye alitajwa kuwa na glovu iliyotengenezwa kwa nakshi za vioo yenye thamani ya $275,000 (£210,000) iliyovaliwa na Michael Jackson.
Licha ya kufanya chaguzi mara kwa mara, hakuna upinzani wa kweli nchini Equatorial Guinea kwani wanaharakati wamefungwa na kukimbilia uhamishoni na wale walio waliosalia hufuatiliwa kwa karibu.
Siasa katika taifa hili zinatajwa kuhusisha fitina za kurithi ikulu na hapa ndipo kashfa inayomhusisha Bwana Engonga inapoingia.
Alikuwa mkuu wa taasisi ya Uchunguzi wa Fedha nchini humo, na alifanya kazi katika kukabiliana na uhalifu kama vile utakatishaji fedha.
Lakini yeye mwenyewe alikuwa chini ya uchunguzi.
Alikamatwa tarehe 25 Oktoba akituhumiwa kwa ubadhirifu wa kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwenye hazina ya serikali na kuziweka katika akaunti ya siri katika Visiwa vya Cayman.
Hajajibu lolote kuhusu tuhuma hizo.
Kisha Bwana Engonga alipelekwa katika gereza maarufu la Black Beach katika mji mkuu, Malabo, ambako inadaiwa kuwa wapinzani wa serikali hutendewa vitendo vyakikatili.
Simu na kompyuta zake zilinaswa na siku chache baadaye video hizo zilianza kuonekana mtandaoni.
Video ya kwanza ambayo BBC imepata kwenye Facebook ni kuanzia tarehe 28 Oktoba kwenye ukurasa wa Diario Rombe, tovuti ya habari inayoendeshwa na mwandishi wa habari aliye uhamishoni nchini Uhispania, ambayo ilisema kwamba "mitandao ya kijamii yashtushwa kwa kuvuja kwa picha na video chafu".
Chapisho kwenye mtandao wa X siku iliyofuata lilitaja "kashfa kubwa iliyotikisa serikali" wakati huu "video za ngono zikimiminika kwenye mitandao ya kijamii".
Teodoro Obiang Mangue (kushoto) alikua makamu wa rais wa nchi
hiyo mwaka 2016.Chanzo cha picha,AFP
Lakini inaaminika kuwa awali walionekana mubashara siku chache mapema kwenye mtandao wa Telegram, kwenye ukurasa mmoja unaojulikana kwa kuchapisha picha za ngono.
Kutoka hapo zilipakuliwa na kushirikiwa katika vikundi vya WhatsApp huko Equatorial Guinea, ambapo zilisababisha taharuki.
Bwana Engonga alitambuliwa haraka pamoja na baadhi ya wanawake katika video hizo, wakiwemo jamaa za rais na wake za mawaziri na maafisa wakuu wa kijeshi.
Serikali haikuweza kupuuza kilichokuwa kikiendelea ambapo tarehe 30 Oktoba Makamu wa Rais Teodoro Obiang Mangue (aliyewahi kuwa mmiliki wa glovu ya Michael Jackson) alizipa kampuni za mawasiliano saa kudhibiti usambazaji wa video hhizo hizo.
"Hatuwezi kuendelea kuangalia tu familia zikisambaratika pasipo kuchukua hatua yoyote," aliandika kwenye mtandao wa X.
"Wakati huo huo,chanzo hasa cha machapisho haya kinachunguzwa ili kupata wachapishaji waliohusika ili kuwawajibisha matendo yao."
Kwa kuwa vifaa vya kompyuta vilikuwa mikononi mwa vikosi vya usalama, tuhuma imemwangukia mtu ambaye, huenda, alitaka kuharibu sifa ya Bwana Engonga kabla ya kesi inayomkabili.
Polisi wametoa wito kwa wanawake kujitokeza kumfungulia kesi Bwana Engonga ya kusambaza picha za faragha bila ridhaa zao.
Mmoja tayari ametangaza kumshtaki.
Jambo ambalo halijabainika ni kwa nini Bwana Engonga alirekodi video hizo.
Lakini wanaharakati wametilia mashaka kile kinachoweza kuwa nia nyuma ya uvujaji huo mkubwa.
Pamoja na kuwa na uhusiano na rais, Bwana Engonga ni mtoto wa Baltasar Engonga Edjo'o, mkuu wa jumuiya ya kiuchumi na kifedha katika eneo hilo, Cemac, na mwenye ushawishi mkubwa nchini humo.
"Tunachoona ni mwisho wa zama,za rais wa sasa, na kuna mengi Zaidi na haya ni masuala ya mvutano wa ndani tunaoshuhudia" alisema mwanaharakati wa nchi hiyo Nsang Christia Esimi Cruz, ambaye sasa anaishi London. .
Akizungumza na BBC Focus on Africa, alidai kuwa Makamu wa Rais Obiang alikuwa akijaribu kumuondoa kisiasa "mtu yeyote ambaye angeweza kupinga urithi wake".
Rais Teodoro Obiang Nguema alipata karibu asilimia 95 ya kura katika uchaguzi uliofanyika miaka miwili iliyopita Chanzo cha picha,AFP
Makamu wa rais, pamoja na mama yake, wanashukiwa kumuengua mtu yeyote anayetishia safari yake ya kuwa rais, akiwemo Gabriel Obiang Lima (mtoto mwingine wa Rais Obiang kutoka mke tofauti), ambaye alikuwa waziri wa mafuta kwa miaka 10 na baadae kuhamishiwa katika jukumu lingine serikalini.
Kwa wale ambao ni mashuhuri wanafikiriwa kufahamu mambo kuhusu wao kwa wao ambayo wangependelea yasiwekwe hadharani,na video zilikuwa zikitumika hapo awali kuwadhalilisha na kuwavunjia heshima wapinzani wa kisiasa.
Pia kuna shutuma za mara kwa mara za kupanga njama za mapinduzi, jambo ambalo linachochea zaidi taharuki.
Lakini Bw Cruz pia anadai kuwa mamlaka inataka kutumia kashfa hiyo kama kisingizio cha kuminya mitandao ya kijamii, ambayo imekuwa chanzo cha taarifa nyingi zinazoendelea ndani ya nchi hiyo kufahamika.
Mnamo Julai, mamlaka ilifunga kwa muda mitandao baada ya maandamano kuzuka katika kisiwa cha Annobón.
Kwake,ukweli kwamba afisa wa ngazi ya juu alikuwa akifanya ngono nje ya ndoa haikushangaza kwani ilikuwa ni sehemu ya maisha machafu ya watu mashuhuri nchini humo.
Makamu huyo wa rais ambaye yeye mwenyewe alihukumiwa kwa ufisadi nchini Ufaransa na kunyang'anywa mali zake katika nchi mbalimbali, anataka aonekane ndiye mtu anayeshughulikia ufisadi na maovu yanayotendwa nchini mwake.
Mwaka jana, kwa mfano, aliamuru kukamatwa kwa kaka yake kwa madai ya kuuza ndege inayomilikiwa na shirika la ndege la nchi hiyo.
Lakini katika kesi hii, licha ya juhudi za makamu wa rais kukomesha kuenea kwa video hizo, bado zinaendelea kutazamwa.
Wiki hii, alionekana akitoa wito wa kufungwa kamera za CCTV katika ofisi za serikali "ili kukabiliana na vitendo vya utovu wa maadili katika ofisi za ummma", shirika moja la habari liliripoti.
Akisema kwamba kashfa hiyo "imedhalilisha taswira ya nchi" aliamuru kwamba maafisa wowote watakaopatikana wakijihusisha na vitendo vya ngono kazini watasimamishwa kazi kwani huo ulikuwa "ukiukaji wa wazi wa kanuni za maadili".
Hakukosea kwamba mkasa huo ulivutia watu wengi kutoka ndani na nje ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Google, maswali yanayotafuta taarifa yakijumuisha jina la nchi hiyo yameongezeka tangu mwanzoni mwa wiki hii.
Siku ya Jumatatu, tarehe X, "Guinea ya Ikweta"
ilikuwa mojawapo ya maneno yanayovuma zaidi nchini Kenya, Nigeria na Afrika
Kusini – kuliko ufuatiliaji wa uchaguzi wa Marekani.
Hili limesababisha baadhi ya wanaharakati ambao wamekuwa wakijaribu kuueleza ulimwengu kuhusu kile kinachoendelea nchini humo wakipatwa na mshangao.
Equatorial Guinea ina changamoto nyingi zaidi kuliko kashfa hii ya ngono," alisema Bwana Cruz, ambaye anafanya kazi katika shirika la kutetea haki liitwalo GE Nuestra.
"Kashfa hii ya ngono kwetu ni dalili tu ya ugonjwa, sio ugonjwa wenyewe. Hii inaonyesha tu namna mfumo ulivyo mbovu."