Rais mteulewa Marekani Donald Trump ameendelea kufanya uteuzi wa wafanyakazi katika serikali yake anaolenga kufanya nao kazi baada ya kuapishwa Januari mwakani.
Kupitia ujumbe kwa vyombo vya habari, Trump amemchagua
mfadhili wake mkuu wa kampeni ambaye pia ni mmiliki wa mtandao wa X Elon Musk
kuongoza idara ya ufanisi wa serikali ya Marekani D.O.G.E.
Elon Musk katika nafasi aliyopewa na rais Donald Trump atashirikiana
na Vivek Ramasway katika kutekeleza majukumu yao katika kipindi cha muhula wa
uongozi wa Trump.
Kwa mujibu wa Trump, amefananisha uteuzi wa wawili hao na “The
Manhattan Project” akisema usimamizi wao utasaidia kupunguza vikwazo vingi, kupunguza
matumizi mabaya ya rasilimali pamoja na
kuchagiza na kufanyia marekebisho mashirika mbali mbali ya serikali.
Mmiliki wa X Elon Musk akikubali kuchukua nafasi hiyo amesema kuwa uteuzi wake
utatikisa sekta mbalimbali za serikali ya Marekani pamoja na mtu yeyote anayehusika
na utumizi mbaya wa serikali ya Marekani.
Uteuzi wa Musk na Vivek ni wa hivi punde kufanywa na Donald
Trump ukijiri siku chache baada ya rais huyo mteule kumteua Sussie Wiles
aliyekuwa mkuu wa kampeni zake katika chaguzi za awali kuchukua nafasi ya mkuu
wa utumishi katika ikulu ya White House.
Trump ameonekana kuwachagua wandani wake wa karibu kama vile
Sussie Wiles na Musk ambao wamekuwa sehemu muhimu kwenye kampeni zake za
kumfikisha ikulu ya White House.
Taarifa za vyombo vya habari nchini Marekani zimeripoti kuwa
Elon Musk alifadhili kampeni ya Trump kwa zaidi ya Dola milioni mia mbili
katika uchaguzi uliofanywa Novemba 5, 2024.