Kulikuwa na zaidi ya maafisa 100 wa polisi wa Korea Kusini na walikuwa na kibali cha kumkamata - lakini wameshindwa kumkamata Rais aliyesimamishwa kazi Yoon Suk Yeol baada ya vute nikuvute ya saa sita nje ya nyumba yake.
Ndio muda ambao makabiliano kati ya timu ya usalama ya Yoon na maafisa hao yalivyodumu, walitengeneza ukuta wa watu na kutumia magari kuziba njia, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.
Amri ya hali ya hatari ya Yoon ilifuatiwa na kura ya kusimamishwa kazi ikafuata. Kisha ukaja uchunguzi wa makosa ya jinai, kukataa kwake kuhojiwa, na sasa amekataa hata kukamatwa, huku akisubiri uamuzi wa mahakama ya kikatiba ambao unaweza kumuondoa madarakani.
Kiongozi huyo wa mrengo wa kulia bado ana wafuasi wengi wanao muunga mkono - na maelfu walijitokeza nje ya nyumba yake Ijumaa asubuhi kupinga kukamatwa kwake.
Walinzi wake
Ingawa Yoon amepokonywa mamlaka yake ya urais - baada ya wabunge kupiga kura ya kumuondoa - lakini bado ana haki ya kupata usalama. Na watu wake wa usalama walichangia pakubwa katika kuzuia kukamatwa siku ya Ijumaa.
Mason Richey, profesa katika Chuo Kikuu cha Hankuk cha Seoul anasema, "ingawa timu ya ulinzi wa rais (PSS) inapaswa kuchukua maelekezo kutoka kwa kaimu Rais Choi Sang-mok. Huenda hawajaagizwa na kaimu Rais Choi kuruhusu akamatwe, au wanakataa maagizo yake."
Baadhi ya wataalam wanaamini walinzi wake huenda wanaonyesha "uaminifu" kwa Yoon, kwa kuwa mkuu wa PSS, Park Jong-joon aliteuliwa kwa kazi hiyo na Yoon Septemba iliyopita.
"Inawezekana Yoon ameweka watu watiifu sana katika timu hiyo katika kujiandaa na tukio hili," anasema mwanasheria mwenye makao yake Marekani na mtaalamu masuala ya Korea, Christopher Jumin Lee.
Na mtangulizi wa Park alikuwa waziri wa zamani wa ulinzi Kim Yong-hyun, ambaye anashutumiwa kwa kumshauri Yoon kutangaza hali ya hatari. Kwa sasa anashikiliwa kwa mahojiano kama sehemu ya uchunguzi wa uhalifu wa Yoon.
Hatari ya mvutano kuongezeka
Suluhu "rahisi", Lee anasema, ni kwa kaimu rais Choi kuamuru PSS iruhusu akamatwe. "Ikiwa hataki kufanya hivyo, hiyo inaweza kuwa sababu na yeye kushtakiwa na Bunge," aliongeza.
Choi, ambaye ni waziri wa fedha, ameshika nafasi hiyo baada ya wabunge kupiga kura ya kumwondoa mrithi wa kwanza wa Yoon, Waziri Mkuu Han Duck-soo.
Mkwamo huu wa kisiasa unaonyesha mgawanyiko katika siasa za Korea Kusini - kati ya wale wanaomuunga mkono Yoon, na uamuzi wake wa kuweka sheria ya hali ya hatari, na wale wanaoipinga.
Idadi kubwa ya Wakorea Kusini wanakubali kwamba tamko la Yoon la sheria ya hali ya hatari Desemba 3 lilikuwa la makosa na anahitaji kuwajibika, anasema Duyeon Kim, mtaalamu wa masuala ya usalama.
PSS pia ina silaha nzito, kwa hivyo maafisa wanaotaka kumkamata rais hawataki mzozo uongezeke.
"Ni nini kitatokea ikiwa polisi watajitokeza na vibali vya ziada vya kutaka kukamatwa kwa maafisa wa PSS, na [PSS] wakakaidi vibali hivyo na kisha kufyatua bunduki zao?" anauliza Lee.
Wakati marais wa Korea Kusini wamefungwa hapo awali, Yoon ndiye wa kwanza kukamatwa kabla ya kujiuzulu. Maafisa wana hadi Januari 6 kumkamata Yoon kabla ya hati ya sasa kuisha.
Wanaweza kujaribu kumkamata Yoon tena mwishoni mwa juma, ingawa wikendi inaweza kuleta changamoto kubwa ikiwa umati wa wafuasi utaongezeka. Wanaweza pia kutuma maombi ya hati mpya na kujaribu kumkamata tena.