Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema zaidi ya wanajeshi 46,000 wa Ukraine wameuawa tangu uvamizi wa Urusi ulipoanza kwa kiwango kikubwa mnamo Februari 2022, huku "makumi ya maelfu wengine wakiwa hawajulikani walipo au wakiwa mateka".
Akizungumza na NBC News Jumapili, Zelensky alisema wale waliotangazwa hawajulikani walipo huenda wamefariki au wako kizuizini nchini Urusi.
Wiki moja na nusu iliyopita (tarehe 6 Februari), Zelensky alisema wanajeshi wa Ukraine waliouawa walifikia 45,100, huku takriban 390,000 wakijeruhiwa. Hata hivyo, wataalamu wa kijeshi wa Ukraine na Magharibi wanaamini idadi halisi inaweza kuwa juu zaidi.
Pia, Zelensky alisema kuwa watoto wa Ukraine wapatao 19,500 wamepelekwa kwa lazima nchini Urusi.
Urusi haijawahi kutangaza idadi ya wanajeshi wake waliopoteza maisha katika vita vya Ukraine, lakini ripoti ya Ujasusi wa Ulinzi nchini Uingereza mnamo Desemba ilikadiria kuwa wastani wa wanajeshi 1,523 wa Urusi wanauawa au kujeruhiwa kila siku.
Zelensky anadai kuwa hadi sasa wanajeshi 350,000 wa Urusi wameuawa, ingawa ripoti nyingine zinasema kuwa idadi hiyo inaweza kuwa kubwa zaidi.