
Milipuko na milio ya risasi iliripotiwa mjini wa Bukavu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Alhamisi, wakati mkutano wa kundi la M23, uliohudhuriwa na kiongozi wa kundi hilo, Corneille Nangaa, kulingana na shirika la habari la AFP.
Bukavu ni mojawapo ya miji muhimu katika mkoa wa Kivu Kusini, ambao umeathiriwa na machafuko ya kisiasa kwa muda mrefu.
Mji huo ulitekwa na wapiganaji wa M23, kundi linalopingana na serikali ya DRC, ambalo linadaiwa kupokea msaada kutoka kwa vikosi vya Rwanda, kwa mujibu wa ripoti za wataalamu wa Umoja wa Mataifa.
Mlipuko wa kwanza uliibua hofu miongoni mwa watu waliokuwa wakihudhuria mkutano huo, na kuwalazimisha kutawanyika haraka.
Muda mfupi baadaye, mlipuko wa pili ulisikika tena katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa waandishi wa AFP waliokuwepo katika eneo la tukio, Corneille Nangaa alikuwa ameondoka kwenye Uwanja wa Uhuru, ambapo mkutano huo ulifanyika, wakati wa milipuko hiyo.
Ghasia na machafuko yanayoshuhudiwa katika maeneo ya mashariki mwa DRC, yamevuruga kwa kiwango kikubwa kwa ustawi wa Congo.
M23 ilichukua udhibiti wa mji wa Bukavu zaidi ya wiki moja iliyopita, baada ya kuiteka Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mashariki mwa DRC, ambayo imekuwa uwanja wa vita vya muda mrefu, sasa inakumbwa na ghasia mpya huku wapiganaji wa M23 wakieneza utawala wao katika mikoa hii.