logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mambo muhimu yanayotarajiwa kutawala mazungumzo ya Donald Trump na Vladimir Putin kuhusu vita Ukraine

Vita baina ya mataifa haya mawili vimekuwepo kwa muda mrefu sasa na chimbuko lake likianza mwezi Feburuari mwaka 2014.

image
na Japheth Nyongesa

Kimataifa18 March 2025 - 10:13

Muhtasari


  • Trump alichapisha taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, akisema atazungumza na Putin siku ya Jumanne asubuhi.
  • Kumekuwa na usiri kutoka ndani ya utawala wa Trump kuhusu jinsi mazungumzo ya kusitisha mapigano yatakavyo kuwa.

caption

Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi wanapanga kuzungumza hii leo Jumanne kuhusu jinsi ya kuafikiana na kukubaliana kusitisha mapigano kati ya nchi ya Urusi na Ukraine.

Vita baina ya mataifa haya mawili vimekuwepo kwa muda mrefu sasa na chimbuko lake likianza mwezi Feburuari mwaka 2014.

Rais wa  Marekani Donald Trump amesema kwamba vipengele vingi vya makubaliano ya amani nchini Ukraine vimekubaliwa na mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin. Trump ameyasema hayo kabla ya mazungumzo yao ya simu yanayotarajiwa leo.

Trump alichapisha taarifa kwenye mtandao wa kijamii wa Truth Social, akisema atazungumza na Putin siku ya Jumanne asubuhi.

Amesema, ingawa kuna makubaliano, lakini mengi ya makubaliano hayo bado hayajafanyiwa kazi.

"Kila wiki kuna vifo vya askari 2,500, kutoka pande zote mbili, na lazima hilo liishe sasa. Ninatarajia mengi katika simu na Rais Putin," Trump aliandika.

Hapo awali aliwaambia waandishi wa habari "tutaona ikiwa tutaweza kufanya makubaliano ya amani, usitishaji vita na amani, na naamini tutaweza kufanya hivyo".

Katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia Jumatatu, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alimshutumu Putin kwa kurefusha vita.

"Pendekezo hili (la kusitisha vita) lingeweza kutekelezwa muda mrefu uliopita," alisema, akiongeza kuwa "kadiri vita vikiendelea, inamaanisha maisha ya binadamu hupotea."

Kumekuwa na usiri kutoka ndani ya utawala wa Trump kuhusu jinsi mazungumzo ya kusitisha mapigano yatakavyo kuwa.

Baadhi ya mambo makuu ambayo yanatarajiwa kwenye mazungumzo ni pamoja na Kusitisha mapigano kwa siku 30, Kinu cha nyuklia, wanajeshi wa Nato pamoja na kuhusu swala la Ardhi ambayo wanaipigania.

Pendekezo la kusaka amani lilijadiliwa na wajumbe wa Ukraine na Marekani nchini Saudi Arabia wiki iliyopita. Baada ya saa kadhaa za kujifungia ndani ya chumba, walitangaza pendekezo la kusitisha mapigano kwa siku 30, na Ukraine ilisema iko tayari kukubali.

Alipoulizwa siku ya Jumapili ni makubaliano gani yatazingatiwa katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, Trump alisema: "Tutazungumza kuhusu ardhi. Tutakuwa na mazungumzo kuhusu mitambo ya kuzalisha umeme."

Pia kuna maswali mengi kuhusu jinsi usitishaji vita utakavyotekelezwa na kufuatiliwa, huku Putin akisema hatakubali wanajeshi wa Nato kwenye eneo hilo.

Putin amesema hatua zake nchini Ukraine zinalenga kulinda usalama wa taifa la Urusi dhidi ya kile anachosema ni nchi za Magharibi zenye uchokozi, hususan upanuzi wa NATO upande mashariki.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved