
TAIFA la Korea Kaskazini ni moja ya mataifa mengi tu katika bara la Asia ambayo yanashuhudia kupungua kwa kasi ya kuzaana ambayo imeathiri ukuaji wa idadi ya watu katika miongo ya hivi karibuni.
"Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani
2024" ya Umoja wa Mataifa inakadiria kuwa kiwango cha kuzaliwa nchini humo
kimepungua polepole kutoka 2.17 katika miaka ya 1990 na 1.92 katika miaka ya
2000, hadi 1.86 katika miaka ya 2010s.
Mnamo 2025, idadi ya watu wa Korea
Kaskazini inakadiriwa kuwa karibu milioni 26.57, na kiwango cha uzazi cha 1.77,
kikionyesha kupungua kwa kiwango cha kuzaliwa na uwezekano wa kupungua kwa
idadi ya watu siku zijazo.
Ni kutokana na data hizi za kuhuzunisha
ambapo washikadau mbalimbali akiwemo rais Kim Jong-Un wamejitokeza na kutoa rai
ya kipekee kwa kina mama wa taifa hilo kushika mimba ili kuokoa kizazi.
Ikumbukwe Desemba 2023, Kim Jong-Un katika
moja ya hotuba zake kwa taifa, alionekana akilia na kufuta chozi wakati
akiwabembeleza wanawake kukubali kuzaa.
Bw Kim alionekana akipapasa macho yake kwa kitambaa
katika wakati adimu wa hisia alipokuwa akihutubia Mkutano wa Kitaifa wa Akina
Mama mjini Pyongyang.
Alionekana kujaribu kuzuia machozi katika
hotuba yake huku akitoa wito kwa wanawake kusaidia kuimarisha nguvu ya taifa.
"Kukomesha kushuka kwa viwango
vya kuzaliwa na kutoa malezi bora ya watoto na elimu ni masuala yetu yote ya
familia ambayo tunapaswa kutatua pamoja na mama zetu," Bw Kim aliambia mkutano.
Wataalamu wanaamini kuwa familia nyingi
mpya hazina zaidi ya mtoto mmoja nchini Korea Kaskazini kwa sababu
"zinahitaji pesa nyingi kulea watoto wao".
Ombi la Bw Kim la kutokwa na machozi ni
tofauti kabisa na mipango ya kudhibiti uzazi iliyoanzishwa na Korea Kaskazini
katika miaka ya 1970s na 80s ili kupunguza kasi ya ongezeko la watu baada ya
vita.
Kisha katikati ya miaka ya 1990s, njaa
ilikadiriwa kuua mamia kwa maelfu ya watu, na kupelekea kiwango cha uzazi
katika nchi hiyo kupungua sana, kulingana na ripoti iliyochapishwa mwezi Agosti
2023 kutoka Taasisi ya Utafiti ya Hyundai yenye makao yake makuu Seoul.