Ndege zisizo na rubani (drones) pamoja na teknolojia ya akili bandia (AI) zinapanuliwa katika matangazo ya Olimpiki za Majira ya Baridi 2026 ili kuboresha uzoefu wa watazamaji, shirika la Olympic Broadcasting Services (OBS) lilisema Jumanne.
Katika michezo kama ya kuteleza kwa kasi kwenye barafu (speed skating), kamera sasa zinawafuatilia wanariadha kwa karibu kutoka nyuma, zikisisitiza kasi na kuleta hisia halisi zaidi za uwanjani. Picha hizo huambatana na sauti hafifu ya mvumo inayotokana si na wapiga picha wa kawaida, bali na drones.
“Tunatumia jumla ya drones 25,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa OBS, Yiannis Exarchos. “Tunazitumia karibu katika michezo yote, isipokuwa hoki ya barafu na mchezo wa curling.”
Exarchos alisema drones hizo zimeboreshwa kulingana na mahitaji ya kila mchezo baada ya majaribio ya kina na uratibu na mashirikisho ya kimataifa ili kuhakikisha usalama na ufanisi. Marubani wa drones pia hupatiwa mafunzo maalum kwa kila mchezo, na baadhi yao wana uzoefu wa moja kwa moja katika michezo husika.
“Baadhi yao ni wanariadha wa zamani wa michezo hiyo, jambo linaloleta tofauti kubwa,” alisema Exarchos. “Wanajua hasa wapi kuna picha bora zaidi.”
Liu Qi wa China akiwa uwanjani wakati wa mashindano ya timu mchanganyiko ya kuruka kwa ski katika Michezo ya Olimpiki za Majira ya Baridi ya Milan-Cortina 2026 huko Predazzo, Italia, Februari 10, 2026. (Xinhua/Meng Yongmin)“Ndani ya shirika, pia tuliomba maoni ya wanariadha,” alisema Exarchos. “Wameunga mkono kwa sababu wanaona picha na matokeo, na wanaelewa maana yake kwa watazamaji kuelewa vizuri kile wanachofanya.”
Zana za akili bandia pia zinaendelezwa zaidi kwa ajili ya Michezo ya Milan-Cortina. Mfumo wa marudio ya picha wa nyuzi 360 ulioanzishwa Beijing 2022 sasa utapatikana katika mashindano yote, ukitumia AI kukokotoa na kuonesha vipimo kama kasi, urefu wa kuruka na idadi ya mizunguko.
“Huu ndio wakati hasa ambao watazamaji wanataka kuelewa kilichotokea,” alisema Exarchos, akiongeza kuwa teknolojia hiyo husaidia kufafanua mwendo, ugumu na utendaji katika muda na nafasi.
Zamani, kuandaa marudio sahihi kama hayo kungechukua saa au hata siku, lakini sasa huchukua takriban sekunde tano tu. Kwa mujibu wa OBS, AI hutenganisha wanariadha na mandhari ya nyuma, kuunda picha za mwendo wa pande tatu na kukokotoa takwimu za utendaji kwa wakati halisi.
Kwa ushirikiano na mshirika wa OBS, Alibaba, jukwaa la uchambuzi wa wakati halisi pia limetengenezwa ili kutambua matukio muhimu kwa kutumia video, sauti, maelezo ya mtangazaji na takwimu.
Exarchos alisema mfumo huo ni muhimu hasa kwa vituo vya matangazo wakati wa mahitaji makubwa ya vipande vya video vya wanariadha nyota, akiongeza kuwa matumizi ya AI na drones yanalenga kusaidia usimulizi wa hadithi badala ya kuonesha teknolojia yenyewe.
“Ni kuhusu wanariadha na Michezo yenyewe,” alisema Exarchos. “Ni kuhusu kusimulia hadithi zao, kuwahusisha watazamaji na kufanya hivyo kwa njia bora zaidi iwezekanavyo.”

Picha hii inaonesha maonesho ya OBS katika Kituo cha Kimataifa cha Matangazo cha Michezo ya Olimpiki za Majira ya Baridi ya Milan-Cortina 2026 mjini Milan, Italia. (Xinhua)
