Tofauti na mwaka uliopita ambapo tukio la kwanza la nusu marathon ya roboti lilivutia umati mkubwa kwa sababu ya upekee wake, safari hii mashine hizo zilikuwa na jukumu kubwa zaidi—kuthibitisha uwezo wao halisi. Katika mwaka mmoja uliopita, roboti za China zimevutia dunia kwa uwezo wao wa kukimbia, kufanya sanaa za kijeshi na hata kucheza. Lakini swali kubwa limekuwa: je, zinaweza kufanya zaidi ya kuwa vifaa vinavyodhibitiwa kwa mbali? Waandaaji wa mbio za kilomita 21.1 za mwaka 2026 waliweka sheria mpya: roboti zisizoweza kujiongoza ziliruhusiwa kushiriki, lakini muda wao wa kumaliza ungeongezwa kwa asilimia 20. Hii ililenga kuhamasisha matumizi ya akili bandia inayojitegemea. Takriban asilimia 40 ya roboti zilishiriki mbio hizo bila msaada wa moja kwa moja. Wahandisi wa China sasa wanazingatia zaidi kuboresha “ubongo” wa roboti—yaani akili bandia—kuliko nguvu za miili yao.
Roboti mwenye umbo la binadamu “Flash” wa timu ya Qitiandasheng katika kundi la kujitegemea akikimbia wakati wa nusu marathon ya Beijing E-Town na mbio za roboti wenye umbo la binadamu katika eneo la Maendeleo ya Kiuchumi na Teknolojia la Beijing kusini mashariki mwa China, Aprili 19, 2026. (Xinhua/Luo Yuan)
Roboti mwenye umbo la binadamu “Unitree H1” wa timu ya Hang S Sai katika kundi la kujitegemea akivuka mstari wa mwisho wakati wa nusu marathon ya Beijing E-Town na mbio za roboti wenye umbo la binadamu katika eneo la Maendeleo ya Kiuchumi na Teknolojia la Beijing kusini mashariki mwa China, Aprili 19, 2026. (Xinhua/Zhang Chenlin)
Tofauti na miundo mbalimbali ya mwaka uliopita, washindani wa mwaka huu walitumia mifumo michache ya kawaida ya roboti, huku ushindani mkubwa ukiwa kwenye programu na algorithimu. Roboti kutoka kampuni ya Honor ndiyo iliongoza, ikiwa na mwendo wa kipekee na muundo wa rangi nyekundu na nyeusi. Hata hivyo, mshindi halisi wa kujitegemea alikuwa roboti nyingine kutoka kampuni hiyo hiyo. Kwa kutumia dakika 50 na sekunde 26, roboti hiyo ilivunja rekodi ya dunia ya binadamu kwa zaidi ya dakika sita. “Tulijifunza kutoka kwa wanariadha bora wa binadamu,” alisema mhandisi Du Xiaodi. Nafasi ya pili na ya tatu pia zilichukuliwa na roboti za Honor zinazojitegemea. Katika tukio la kuvutia, roboti moja haikuweza kusimama kwa wakati na kugonga uzio wa usalama, hali iliyowafanya watazamaji kushangilia na kushituka kwa pamoja. Roboti ya Tien Kung Ultra, ingawa haikuingia tatu bora, ilivutia kwa mbio zake za mwisho ambapo ilimpita mpinzani wake kwa ustadi mkubwa na kumaliza kwa saa 1 na dakika 15—ikiwa ni maboresho makubwa kutoka saa 2 na dakika 40 mwaka 2025. Mhandisi Zhao Wen alieleza mafanikio hayo kuwa yametokana na maboresho ya akili bandia inayounganisha mifumo ya udhibiti, mawasiliano na utambuzi.
Roboti mwenye umbo la binadamu “Tiangong 1.0 Ultra” (kushoto) wa timu ya Tianxiao katika kundi la kujitegemea akikimbia wakati wa nusu marathon ya Beijing E-Town na mbio za roboti wenye umbo la binadamu katika eneo la Maendeleo ya Kiuchumi na Teknolojia la Beijing kusini mashariki mwa China, Aprili 19, 2026. (Xinhua/Zhang Chenlin)
Mbio hizo zilikuwa changamoto kubwa kwa roboti, zikijumuisha aina zaidi ya 10 za ardhi, miteremko ya hadi asilimia 8, pamoja na kona 22 kali zilizohitaji usahihi wa hali ya juu.
Roboti mwenye umbo la binadamu “X1” (kulia, mbele) wa timu ya Pofengzhe katika kundi linalodhibitiwa kwa mbali akikimbia wakati wa nusu marathon ya Beijing E-Town na mbio za roboti wenye umbo la binadamu katika eneo la Maendeleo ya Kiuchumi na Teknolojia la Beijing kusini mashariki mwa China, Aprili 19, 2026. (Xinhua/Luo Yuan)
“Kujiendesha katika mazingira kama haya ni kipimo kikubwa cha uwezo wa roboti,” alisema mtafiti Zhao Mingguo wa Chuo Kikuu cha Tsinghua. Licha ya mashindano hayo kuisha, safari halisi bado inaendelea. Wataalamu wanaamini roboti hazikusudiwi kuchukua nafasi ya binadamu moja kwa moja, bali kusaidia katika kazi hatarishi au ngumu.
Mfanyakazi wa kampuni ya roboti akirekebisha roboti mwenye umbo la binadamu katika kampuni ya roboti mjini Shenzhen, mkoa wa Guangdong kusini mwa China, Juni 25, 2025. (Xinhua/Li An)
Katika mji wa Shenzhen, roboti tayari zinatumika katika shughuli mbalimbali kama kuongoza trafiki na kufanya kazi za nyumbani. Kwa mujibu wa makadirio, soko la roboti wenye umbo la binadamu nchini China linaweza kufikia yuan bilioni 870 ifikapo mwaka 2030. “Roboti hawakimbii kwa ajili ya mbio tu,” alisema Liang Liang wa Taasisi ya Elektroniki ya China. “Lengo ni kukuza ubunifu wa teknolojia na kuleta matumizi halisi sokoni.”
