Fahamu kampuni ya Naomi Osaka na Lebron James 'Hana Kuma' iliyozua mdahalo Kenya

Muhtasari

•Habari kutoka Marekani zinasema kampuni hiyo  inalenga kusimulia hadithi zinazovuka kizuizi cha kitamaduni.

•Hana Kuma kwa Kijapani linamaanisha 'Zaa ua'. Neno 'Hana' kwa Kijapani linamaanisha 'Ua' na 'Kuma' linamaanisha 'Zaa'. 

Image: INSTAGRAM// NAOMI OSAKA

Mchezaji tenisi wa kimataifa wa Japan Naomi Osaka ameshirikiana na mchezaji wa mpira wa vikapu wa Marekani Lebron James kuanzisha kampuni ya habari.

Wanariadha hao wawili  mahiri walitangaza uzinduzi wa kampuni ya Hana Kuma siku ya Jumanne.

Habari kutoka Marekani zinasema kampuni hiyo  inalenga kusimulia habari kemkemu  zinazovuka kizuizi cha kitamaduni.

Kulingana na ripoti kutoka Hollywood, Hana Kuma, itatoa simulizi ambazo "ni maalum za kitamaduni lakini za kimataifa kwa watazamaji wote" na tayari imepanga miradi mingi.

"Katika enzi ya utiririshaji, yaliyomo yana mtazamo wa kimataifa zaidi. Unaweza kuona hili katika umaarufu wa televisheni kutoka Asia, Ulaya na Amerika ya Kusini kwamba mambo ya kipekee yanaweza pia kuwa ya ulimwengu wote. Hadithi yangu ni ushahidi wa hilo pia. Nimefurahia sana kile tunachojenga huko Hana Kuma. Tutaleta hadithi tukiwa na lengo hili akilini: kufanya mitazamo ya kipekee kuwa ya ulimwengu wote na kuwatia moyo watu njiani," Osaka alisema wakati akiwahutubia waandishi wa habari.

Hana Kuma kwa Kijapani linamaanisha 'Zaa ua'. Neno 'Hana' kwa Kijapani linamaanisha 'Ua' na 'Kuma' linamaanisha 'Zaa'. Wakenya hata hivyo wamelitafsiri neno hilo kimakosa kwani lina maana tofauti kabisa katika Kiswahili.

Osaka ambaye amezaliwa na baba wa asili ya Haiti na Japan ni  miongoni mwa wanaspoti mabwenyenye zaidi duniani.

Kulingana na Forbes, Osaka aliibuka kuwa mwanaspoti wa kike anayelipwa pesa nyingi zaidi ulimwenguni mwaka 2020 kwa kuzoa jumla ya dola milioni 37 kutokana na orodha ndefu ya mikataba ya udhamini.