"Nililala na mama yake sio mvulana," mshukiwa wa ulawiti aambia mahakama

Muhtasari

• Japheth Kiprotich alifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa Kibera William Tullen kujibu shtaka la kumlawiti mvulana wa umri wa miaka tisa. 

Japheth Kiprotich mbele ya hakimu mkazi wa Kibera William Tullen, Jumatano, Mei 4, 2022 Picha: CLAUSE MASIKA
Japheth Kiprotich mbele ya hakimu mkazi wa Kibera William Tullen, Jumatano, Mei 4, 2022 Picha: CLAUSE MASIKA

Mwanamume mmoja siku ya Jumatano aliishangaza mahakama ya Kibera baada ya kudai kuwa alilala na mama wa mtoto wa miaka tisa ambaye anadaiwa alimlawiti. 

Japheth Kiprotich alifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa Kibera William Tullen kujibu shtaka la kumlawiti mvulana wa umri wa miaka tisa. 

Alikanusha mashtaka na kuiambia mahakama kuwa alikuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mamake mvulana huyo. 

"Nililala na mama yake pekee wala sio mvulana mdogo kama wanavyodai," Kiprotich alisema. 

Alipuuzilia mbali mashtaka hayo akisema ni ya nia mbaya na kuitaka mahakama kutupilia mbali kesi hiyo. 

Waendesha mashtaka wa serikali Jane Gitai na Ann Wanjiku hawakupinga kuachiliwa kwa Kiprotich kwa bondi lakini waliitaka mahakama kumpa masharti magumu wakisema kosa hilo ni kubwa. 

Kulingana na stakabadhi za mashtaka Kiprotich alitenda kosa hilo Aprili 30 eneo la Southlands katika kaunti ndogo ya Lang'ata, Kaunti ya Nairobi. 

Inadaiwa alitembelea nyumba ya mtoto huyo na kumshawishi alale sakafuni kabla ya kumlawiti. 

Mvulana huyo hakuweza kupiga kelele kuomba msaada kwani inasemekana mshitakiwa alikuwa ameziba mdomo wake kwa kitambaa. 

Kiprotich pia alikanusha shtaka lingine la kufanya kitendo kichafu na mtoto mdogo. 

Mahakama ilimwachilia kwa bondi ya Shilingi laki tatu au dhamana ya shilingi laki moja pesa taslim. Kesi hiyo itatajwa Mei 10.