Uhuru amsimamisha kazi Jaji Said Chitembwe

Muhtasari

• Rais alitangaza kuunda jopo maalum kumchunguza Chitembwe kuambatana na pendekezo la Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) iliyopendekeza jaji huyo achunguzwe. 

• Maombi manne yaliwasilishwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, Francis Wambua, Imgrad Geige na David Leboo Ole Kilusu wakitaka aondolewe. 

• Tume ya JSC iliamua kwamba maombi yaliyowasilishwa kutaka Chitembwe kufurushwa yaliwasilisha sababu za kutosha za kuondolewa kwake. 

Jaji Said Juma Chitembwe wakati wa mahojiano kwa nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Juu Mei 3. Picha: CHARLENE MALWA
Jaji Said Juma Chitembwe wakati wa mahojiano kwa nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Juu Mei 3. Picha: CHARLENE MALWA

Rais Uhuru Kenyatta amemsimamisha kazi jaji wa Mahakama ya kuu Said Chitembwe ili kutoa nafasi kufanyika kwa uchunguzi dhidi yake kuhusu madai ya utovu wa nidhamu uliokithiri. 

Rais Kenyatta pia alitangaza kuunda jopo maalum kumchunguza Chitembwe kuambatana na pendekezo la Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) iliyopendekeza jaji huyo achunguzwe. 

Jopo hilo litaongozwa na Jaji Mumbi Ngugi huku wanachama wengine wakijumuisha Wakili Dkt. Fred Ojiambo, Jaji Abida Ali Aroni, Jaji Nzioki wa Makau, James Ochieng' Oduol, Luteni Jenerali mstaafu Jackson W. Ndung'u na Lydia Nzomo. Wakili mkuu katika jopo hilo atakuwa Wakili Kiragu Kimani akisaidiana na Joseph Gitonga Riungu na Edward Omotii Nyang’au huku Makatibu wakiwa Jasper M. Mbiuki na Sarah Yamo. 

Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) iliamua kwamba maombi yaliyowasilishwa kutaka Jaji Said Chitembwe aondolewe ofisini kwa misingi ya utovu wa nidhamu yaliwasilisha sababu za kutosha za kuondolewa kwake. 

Maombi manne yaliwasilishwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko, Francis Wambua, Imgrad Geige na David Leboo Ole Kilusu wakitaka Jaji huyo aondolewe afisini. 

Walalamishi hao walimshtumu jaji huyo kwa kuhusika katika utoaji hongo katika mzozo wa ardhi ambayo alishughulikia.