Kibwana amtaka Kalonzo kuacha msimamo mkali na kurejea Azimio

Muhtasari

• "Hakuna madai zaidi yasiyo na mwisho," Kivutha alisema.

• Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana amekitaka chama cha Wiper kuacha matakwa yake yasiyoisha na kurejea katika muungano wa Azimio la Umoja.

 

Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana
Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana
Image: HISANI

Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana amekitaka chama cha Wiper kuacha matakwa yake yasiyoisha na kurejea katika muungano wa Azimio la Umoja.

Katika ukurasa wake wa Twitter Alhamisi, Kibwana alisema chama cha Wiper bado kitakuwa na nafasi ya kujadiliana na vyama vingine kutoka Ukambani ili kujumuishwa katika utawala wa Azimio iwapo chama hicho kitatwaa kiti cha urais baada ya uchaguzi wa Agosti.

“Waita Nzioka, Charity Ngilu na mimi bado tunakaribisha Wiper kwa Azimio. Hata hivyo, vyama vyote vinavyomfanyia kampeini The 5th  Ukambani vitakaa na mgombeaji na naibu wake ili kuafikiana kuhusu maendeleo na sura ya serikali ya eneo hili,” Kibwana alisema.

"Hakuna madai zaidi yasiyo na mwisho," aliongeza.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka Jumapili iliyopita alitangaza kwamba chama hicho kilikuwa kimekatiza uhusiano na Azimio la Umoja baada ya nafasi ya mgombea mwenza kupewa kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua.

Kalonzo alitangaza kuwa atawania urais mwenyewe na kumtambulisha Andrew Sunkuli kama mgombea mwenza wake.

Kibwana alihama Wiper mwezi Agosti 2021 baada ya kutofautiana na Kalonzo na kujiunga tena na Muungano Party, chama kinachounga mkono Azimio.

Wito wake kwa chama cha Wiper, na kwa jumla, kwa Kalonzo kuacha kutoa matakwa kwa Azimio ulitoa shinikizo kwa Makamu huyo wa Rais wa zamani kufikiria upya uamuzi wake wa kuondoka Azimio.

Hii ni baada ya mwaniaji naibu gavana wa Azimio Nairobi, Philip Kaloki, kusema mgombea wake wa urais bado ni Raila Odinga.

Kaloki, ambaye ni mwanachama wa chama cha Kalonzo cha Wiper, alisema Alhamisi kwamba hawajaombwa kuacha kumuunga mkono mgombeaji urais wa Azimio.

Alisema makubaliano ya awali katika Azimio kwa Jubilee na Wiper kutoa wagombeaji wa ugavana na naibu gavana wa kiti cha juu cha Nairobi bado yana yatasalia.

"Hatuna mwelekeo wowote kinyume na msimamo huu," Kaloki alisema kwenye K24 TV.

Mnamo Mei 9, mgombea ugavana wa Machakos Nzioka Waita alimtaka Kalonzo kuacha msimamo wake mkali kuhusu wadhifa wa naibu wa Azimio la Umoja.

Waita alimtahadharisha kinara huyo wa Wiper kwamba itikadi yake ya 'njia yangu au barabara kuu' ('my way or the highway') ina hatari ya kuitenga jamii ya Wakamba katika upinzani baada ya uchaguzi wa Agosti.

"Iwapo Azimio atashindwa na uhuni huu, ni bora sisi jamii ya Wakamba tuweke kiti cha mapema kwenye viti vya upinzani ambapo tutakaa kwa miaka 10 zaidi," alisema.