Mwanamume afikishwa mahakamani kwa kuoa msichana wa miaka 13

Alisema hakujua ni kinyume cha sheria kuoa msichana wa umri mdogo chini ya mila za Kimasai.

Muhtasari

• Msichana huyo ambaye ni mtoro wa shule alikuwa ameambia mahakama jinsi alivyoanza mapenzi na mshtakiwa

Mahakama
Mahakama

Mwanamume mwenye umri wa miaka 24 amekiri mbele ya mahakama ya Loitoktok kwamba hakujua kuwa ni kinyume cha sheria kuoa msichana wa umri mdogo chini ya mila za Kimasai.

Justine Marau katika utetezi wake alimwambia Hakimu Mkuu Judicaster Nthuku kwamba alitoroka na msichana, mwenye umri wa miaka 13, na kumuoa kulingana na mila za Kimasai. Hata hivyo, Hakimu alisema Katiba inazidi sheria nyingine yoyote ile ikiwemo kanuni za utamaduni.

Marau alitenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2020 na Mei 1, 2021 katika Wadi ya Kuku katika Kaunti Ndogo ya Loitoktok. Msichana huyo ambaye ni mtoro wa shule alikuwa ameambia mahakama jinsi alivyoanza mapenzi na mshtakiwa alipokuwa akifanya kazi katika duka lake mwaka 2020. Mwezi Desemba mwaka 2021 aligundua kwamba alikuwa mjamzito na alipomjulisha mshtakiwa, alitoroka naye hadi Kaunti Ndogo ya Mashuru ambako walikuwa wakiishi kama wanandoa.      

       

Nantoye ole Kiruti, mamake msichana huyo alikuwa ameambia mahakama jinsi mnamo Machi 24 alifika nyumbani na kumpata bintiye hayupo. Aligundua baadaye kwamba mshtakiwa ambaye alikuwa amemwajiri mtoto huyo katika duka lake alikuwa ametoroka naye na kumfanya mkewe. Aliandikisha ripoti katika kituo cha polisi cha Ilasit kabla ya kuwasiliana na mshtakiwa ambaye alithibitisha kuishi na msichana huyo.

Chifu wa eneo la Nkama katika Kata ya Kuku Robert Mintei aliiambia mahakama jinsi Mei 2, 2022 alikutana na mshtakiwa ambaye alimtambulisha msichana huyo kuwa mke wake kabla ya kumjulisha mamake msichana ambaye alithibitisha kupokea ripoti hiyo kutoka kwa mshtakiwa. Siku iliyofuata, mshtakiwa alikamatwa na kufunguliwa mashtaka kabla ya kufikishwa mahakamani ambapo alikana mashtaka hayo.

Mahakama ilipanga Julai 21 kwa ajili ya kutoa hukumu.