Hatimaye sababu za kucheleweshwa kwa Visa ya Omanyala zafichuliwa

AK imesema Omanyala aliandamana na wanariadha wenzake kuadikisha Visa ila yake haikutoka pamoja na ya wengine.

Muhtasari

•AK imeeleza kuwa Visa ya mwanariadha huyo ilichelewa kutoka kwani kuna fomu ya ziada ambayo alihitajika kujaza.

•AK imeweka wazi kuwa kesi ya Omanyala ilikuwa zaidi ya wao kuingilia kati kwani kila mwanariadha alihitajika kupitia mchakato wa ombi la Visa mwenyewe.

akishiriki mashindano ya dunia huko Oregon
Bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala akishiriki mashindano ya dunia huko Oregon
Image: TWITTER// FERDINAND OMANYALA

Shirika la wanariadha nchini (AK) limepuuzilia mbali madai kuwa Visa ya bingwa wa Afrika katika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala ilicheleweshwa baada ya mtu mwingine kuchukua nafasi yake.

Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu, AK ilieleza kuwa Visa ya mwanariadha huyo ilichelewa kutoka kwani kuna fomu ya ziada ambayo alihitajika kujaza. Shirika hilo lilibainisha kuwa Omanyala aliandamana na wanariadha wenzake kuadikisha stakabadhi hiyo.

"Wengine walipewa Visa yao siku moja baadae lakini ya Omanyala haikutolewa.  Alihitaji kujaza fomu za ziada zinazojulikana kama 'maswali ya nyongeza kwa waombaji wa Visa', ili kuthibitisha ukweli fulani," Taarifa ya AK ilisoma.

Shirika hilo liliweka wazi kwamba lilifanya majaribio kwa ajili ya Mashindano ya Dunia yanayofanyika Oregon mnamo Juni 24 na 25 na hatimaye kuchagua kikosi cha wanariadha  na maafisa 80.

Baada ya kuchagua kikosi shirika lilitafuta huduma za kampuni ya wataalamu wa nje kushughulikia usajili wa Visa kwa wajumbe wote unaosafiri ili kuhakikisha mchakato mzuri bila changamoto.

AK imeweka wazi kuwa kesi ya Omanyala ilikuwa zaidi ya wao au wizara ya michezo kuingilia kati kwani kila mwanariadha alihitajika kupitia mchakato wa ombi la Visa mwenyewe. Pia imedokeza kuwa bingwa huyo alipokea Visa yake kufuatia juhudu za waziri wa michezo Amina Mohamed.

"Shirika la Riadha Kenya lingependa kutambua juhudi za Amb Amina Mohamed,Waziri wa Michezo, kwa kushirikisha Ubalozi wa Marekani kuandaa Visa," AK ilisema.

Shirika hilo pia limepuuzilia mbali madai kuwa maafisa 32 wa serikali walisafiri pamoja na wanariadha wanaoshiriki mashindano ya dunia nchini Marekani.

AK imeweka wazi kuwa ni maafisa watatu pekee wa serikali ambao waliandamana na wanariadha wanaowakilisha nchi.

"Wizara imeweka sera kali inayohakikisha kuwa ni maafisa walio na majukumu mahususi pekee wanaoandamana na timu kuenda nje ya nchi, jukumu ambalo limekabidhiwa kwa Riadha Kenya baada ya kupatiwa muhtasari wa kina kutoka kwa wizara," Taarifa ilisoma.