Waziri Tuya alinifukuza kwa nyumba, aliyekuwa mumewe adai

Stephen Kudate anadai kuwa Tuya alimtenga kimakusudi kushiriki katika utunzi wa watoto wao.

Muhtasari

• Tuya alifikishwa kortini Oktoba mwaka huu akitaka matunzo ya watoto wao wawili na jumla ya Sh3.1 milioni kila mwaka kwa ajili ya kuwatunza. 

Waziri wa mazingira na misitu Soipan Tuya.
Waziri wa mazingira na misitu Soipan Tuya.
Image: maktaba

Aliyekuwa MCA wa Narok Stephen Kudate amedai kwa hisia kwamba Waziri wa Mazingira Soipan Tuya alimfukuza katika nyumba yao ya ndoa iliyoko mtaani Kileleshwa, Nairobi punde tu alipoteuliwa kuwa waziri. 

Kudate anasema walifunga ndoa kihalali wakiwa wamefuata taratibu zote za ndoa za kitamaduni lakini mnamo Septemba 2022, Tuya alitoroka nyumba yake ya ndoa alipoapishwa kuwa waziri. 

Kudate akijibu ombi lililowasilishwa na Tuya la kutaka matunzo na malezi ya mtoto amekana kuwatelekeza watoto wao.Anadai CS alimtenga kimakusudi kushiriki katika utunzi wa watoto wao. 

“Kama kichwa cha familia, nilikuwa mtu na raslimali za kutosha kutunza wanangu, naye anajua kwamba sina kazi, lakini kwa kile kidogo nilicho nacho, ninatimiza jukumu langu la mzazi kwa njia ifaayo,” asema. 

Tuya alifikishwa kortini Oktoba mwaka huu akitaka matunzo ya watoto wao wawili na jumla ya Sh3.1 milioni kila mwaka kwa ajili ya kuwatunza. Tuya alidai mumewe waliyeachana naye huwatendea ukatili watoto wao na wafanyakazi wake wa nyumbani.

Alisema wamekuwa wakinyanyaswa kisaikolojia, kihisia na matusi na mumewe wa kitambo maana anataka malezi kamili ya watoto hao. Lakini Kudate katika majibu yake alikanusha madai ya unyanyasaji, akisema Tuya ndiye ambaye amekuwa mkali wa maneno na mkorofi.

 “Nimemtunza. Ana nia ya kunikatisha tamaa na kuharibu maisha yangu kama alivyofanya kwa mume wa kwanza kutoka Kajiado, ambaye alimchukua kwa Shahada yake ya Uzamili ya Sheria nchini Marekani na kisha kumtelekeza na kumtupa,” asema. 

Ameiomba mahakama kutotoa maagizo yaliyoombwa na Tuya. Utetezi wake ni kwamba yuko katika nafasi nzuri ya kuishi na watoto wake kwa sababu Tuya hayuko nyumbani kila mara kuzungumza nao.

"Safari zake nyingi za ndani na nje ya nchi zinawaweka watoto kwenye upweke na kutelekezwa. Wanakosa malezi na mwongozo wa wazazi na sura ya baba kwani wamelazimika kuishi na wageni, madereva, wasaidizi wa nyumbani na ndugu kwa sababu ana muda mchache nao,” alisema. 

Kulingana na stakabadhi za mahakama, Tuya alikubali kumuoa Kudate hata akiwa na ufahamu juzi wa kuwepo kwa mke mwingine alipokuwa kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kaunti ya Narok. 

Kudate anasema yuko tayari kuchukua vipimo vya DNA ili kuthibitisha ikiwa watoto wote ni wake. Wawili hao kulingana na Kudate pia wana kesi ya talaka mahakamani.