Mgomo utaendelea hadi matakwa yatimizwe, madaktari wa Mombasa wasimama kidete

Mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru alikuwa amewaamuru madaktari kusitisha mgomo na kurejea kazini la sivyo wahukuliwe hatua za kinidhamu.

Muhtasari

• Dkt Ghalib Salim anayewakilisha tawi la Pwani alikariri msimamo wao akieleza kuwa hawatatii agizo lililotolewa na Baraza la Magavana Jumatano. 

Madaktari waandamana katika barabara ya Ngong kuelekea wizara ya Afya mnamo Machi 22, 2024. Picha: MAKTABA
Madaktari waandamana katika barabara ya Ngong kuelekea wizara ya Afya mnamo Machi 22, 2024. Picha: MAKTABA

Madaktari mjini Mombasa wamethibitisha kuwa hawatarejelea majukumu yao hadi matakwa yao yatakaposhughulikiwa. 

Akizungumza wakati wakiandamana mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Dkt Ghalib Salim anayewakilisha tawi la Pwani alikariri msimamo wao akieleza kuwa hawatatii agizo lililotolewa na Baraza la Magavana Jumatano. 

Mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru alikuwa amewaamuru madaktari hao kusitisha mgomo unaoendelea Jumatano na kurejea kazini la sivyo wahukuliwe hatua za kinidhamu. 

"Hatutarudi nyuma hadi matakwa yetu yatimizwe. Tunakataa kutishiwa, ikiwa wanataka turudi kazini wanapaswa kuzingatia madai yetu," Salim alisema. 

Salim alisema kuwa maazimio yaliyotolewa na mwenyekiti wa CoG hayafanyi kazi kulingana na makubaliano ya CBA. 

"Tuna CBA moja pekee ambayo ni halali kuanzia 2017 hadi 2021, kwa hivyo hawawezi kutuambia twende kaunti tofauti ili CBA yetu isainiwe," Salim alisema. Aliongeza kuwa jukumu la kulinda maisha sio tu kwa madaktari lakini pia kwa magavana. 

"Magavana pia wamekula kiapo kulinda maisha na watu wa nchi hii," Salim alisema. 

Waiguru siku ya Jumatano alisisitiza haja ya kutii maagizo ya mahakama yaliyotolewa Machi 13 na 15 ambayo yalisitisha mgomo huo ili kufanikisha mazungumzo. Akihutubia wanahabari baada ya kikao maalum, mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru, hata hivyo, alijiepusha na kuwajibika kwa jumla kuhusu suala hilo badala yake alikataka kaunti husika kuwachukulia hatua madaktari. 

"Tunatoa wito kwa madaktari walio kwenye mgomo kurejea kazini... ambapo kaunti husika ambazo ni waajiri wao zitakuwa huru kuchukua hatua zozote zinazofaa," Waiguru alisisitiza. 

Gavana huyo wa Kirinyaga alitoa wito kwa madaktari hao kukubali nia njema ambayo imetolewa kwao na serikali ya kitaifa na kaunti kufanya mazungumzo. Alikariri kuwa mazungumzo yanaweza tu kufanywa katika kiwango cha kaunti. 

Mgomo huo unaingia siku ya 15 leo huku madaktari wakitaka kutekelezwa kwa ahadi nyingi, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya pamoja yaliyotiwa saini mwaka 2017. Malalamiko yao ni kucheleweshwa kutumwa kwa wahitimu, malipo ya haki ya wahitimu, mafunzo ya uzamili, ajira ya madaktari zaidi na bima ya afya kwa madaktari.