Mahakama ya Kibera imemhukumu kifungo cha miaka 30 mwanamume mmoja aliyeshtakiwa kwa hatia ya kumuua mwanamke aliyedaiwa kuwa mke wake wa zamani mnamo mwaka wa 2018.
Katika kesi iliyowasilishwa mahakamani humo, upande wa mashtaka ulidhibitishia mahakama kwamba mshukiwa alimuua mwanamke mwenye umri wa miaka 24 aliyekuwa mpenzi wake zamani.
Mmoja wa mashahidi katika kesi hiyo aliiambia mahakama kuwa, mshukiwa alitekeleza kisa hicho baada ya kugundua kwamba marehemu alikuwa anapanga kufunga ndoa na mwanamume mwingine. Shahidi huyo aliendelea kueleza kwamba mshukiwa alimshurutisha marehemu kurejesha zawadi alizokuwa amempa wakati walikuwa kwenye mahusiano.
Mahakama ilielezwa kwamba mshukiwa alimdunga marehemu kwa kisu baada ya mzozo kuibuka baina ya wawili hao wakati marehemu alisita kurejesha zawadi zilizokuwa zinadaiwa na mshukiwa.
Upande wa mashtaka ulieleza mahakama kwamba mshukiwa alikamatwa na umati wa watu waliokuwa wamesikia mayowe kutokakwenye sehemu ya tukio.
Aidha, wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, kwa mujibu wa ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma ODPP, familia ya marehemu ilieleza mahakama kwamba, kifo cha mpendwa wao kimekuwa pigo kubwa kwa wanafamilia kwani marehemu alikuwa sehemu katika familia yake mbali na kuwa mtu mwenye heshima na siku za usoni zilizo bora.
Aidha katika uamuzi wa mahakama, jaji alikiri kwamba
mshukiwa hakuwa na huruma kuhusu kisa kilichotokea na kwamba alikuwa alikana
madai dhidi yake akikiri kwamba marehemu alijidunga kisu.
Hukumu ya miaka 30 jela ilijiri baada ya
ushahidi wa mashahidi 5 kuelezea mahakama matukio yaliyosababisha kifo cha
mwanamke huyo.