Janga la Covid-19, masaibu ya mtoto wa kike

Muhtasari

• Wasichana wengi wamepachikwa mimba kutoka na chagamoto hizi.

• Wengi wameshawishiwa na wanaume waliyojifanya wasamaria wema.

 

Wanafunzi. Picha:MAKTABA
Wanafunzi. Picha:MAKTABA

Katika karne ya 21, ni matarajio ya wengi kwamba changamoto nyingi zilizokuwa zikiwakumba wanadada miongo kadhaa iliyopita zingekuwa zimetatuliwa na kupewa nafasi sawa kujiendeleza kimaisha na kuafikia azma zao maishani.

Bila shaka hatua muhimu zimepigwa ili kuendeleza mwanadada na kumwimarisha kimaisha, hata hivyo bado kuna changamoto nyingi ambazo hazijatatuliwa, na hali imekuwa mbaya zaidi wakati huu wa janga la COVID.

Huku takwimu zikionyesha kwamba mimba za mapema miongoni mwa wasichana wa shule zimeongezeka maradufu wakati huu wa Covid-19 ikilinganishwa na takwimu za awali nchini, tunabaki tukijiuliza tatizo liko wapi?.

 

Ni dhahiri shahiri kwamba wakenya wengi wanaishi katika hali ya uchochole na umaskini ulioganda, hivyo basi katika hali hii wasichana wanajipata katika hali ngumu huku baadhi yao wakiamua kuolewa mapema ili wapate angalau kumudu mahitaji yao.

Shule zilipofungwa kutokana na janga la korona, wasichana wengi haswa wanaotoka familia fukara waliozwa ili wazazi wao wapate hela za kugharamia mahitaji ya  ndugu zao wadodo.

Kutokana nahali zao kiuchumi wengi wao pia wamekuwa mawindo rahisi kwa wanaume wenye hulka mbovu na wenye tabia za kuvizia wasichana wadogo, wanaojifanya wasamaria wema, kumbe ni mbwa mwitu waliyovalia ngozi ya kondoo.

Kuongeza msumari moto kwenye kidonda wengi wametungwa mimba na hata jamaa zao wanaoishi nao nyumba moja. Matendo ambayo tunakashifu na kukemea sana, wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Vile vile, mashirika mengi ya kuwapa misaada wasichana, yalikuwa yanafanikiwa kufanya hivyo wakati wakiwa shuleni, kwa sasa imekuwa vigumu kwa mashirika hayo kufanya hivyo kwa sababu ni vigumu kupata wasichana wakiwa nyumbani ili kuwapa misaada kama vile ya sodo na bidhaa zinginezo.

Katika karne hii ya 21 , bado tunashuhudia wasichana wetu wakikosa bidhaa hizi ambazo ni muhimu sana kwao. Wasichana wengi wamezamia kazi za nyumbani na hata vibarua na wamekosa usaidizi huu wa kimsingi.

Ni changamoto kwa wahudumu wa mashirika haya kuingia katika kila nyumba wakiwatafuta wasichana kwa minajili ya kuwasaidia. Ni changamoto kama hizi ambazo zinazoweza kuchochea msichana kuamua kuolewa ili kupata mtu wa kugharamia mahitaji yake.

 

Wasichana wetu wanapitia changamoto chungu mzima wakati huu.Wengine kwa sababu ya hali zao za uja uzito wataona haya kurejea shuleni kwa hofu ya kuchekwa na kufanyiwa utani. Wengi wao wenasongwa na mawazo wasijuwe cha kufanya.

Wakati umewadia kwa jamii kwa jumla kushirikiana ili kumsaidia mtoto wa kike kujikwamua kutoka minyororo ya Covid-19. Ni jukumu la serikali sio tu wasamaria wema na mashirika ya kibinafsi kuwapa misaada.

Mwandishi Sairin Lupia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mhariri: Davis Ojiambo.