Mwaka mpya mambo mapya lakini changamoto ni zile zile

Muhtasari

  • Janga la korona lilivuruga mipango mingi.

  •  Wengi walipoteza ajira na shule kufungwa. 

Wachuuzi wa mitumba wakiendesha shughuli zao mjini Nairobi. Shughuli zao ziliathirika sana kutokana na janga la COVID-19.
Wachuuzi wa mitumba wakiendesha shughuli zao mjini Nairobi. Shughuli zao ziliathirika sana kutokana na janga la COVID-19.
Image: Maktaba

Huku tukianza mwaka mpya changamoto za mwaka uliyopita bado zipo. Kwa wengi mwaka mpya humaanisha mwanzo mpya na nafasi mpya za kujiimarisha.

Sio siri mwaka uliyopita ulikuwa mwaka wa huzuni na wenye changamoto si haba. Kuanzia kwa maelfu kupoteza kazi, shule na vyuo kufungwa na masomo kuhamishiwa mitandaoni bila kusahau kuongezwa kwa karo za vyuo vikuu. Licha ya mwaka mpya kung’oa nanga changamoto za mwaka uliyopita bado zatukodolea macho.

Cha kuhuzunisha ni kwamba mwaka huu unaonekana utasheheni siasa, huku kura ya maamuzi ikirindimwa ili kufanikisha mchakato wa BBI. Hofu kuu ni kwamba viongozi wetu kama kawaida yao watasahau kila jambo na kuangazia tu kura ya maamuzi.

 

Kile viongozi wetu hawafahamu ni kwamba mwaka huu tunawahitaji zaidi, tunahitaji ajira sio mirindimo ya kisiasa. Tusikubali kutawaliwa na akili za ngiri ambaye husahau hata akikimbizwa na simba na kuwaunga mkono katika siasa mbovu, bali tuendelea kuwakumbusha kuhusu majukumu yao katika kubuni sera za maendeleo.

Wanafunzi wamerejea shuleni baada ya takriban mwaka mzima nje ya shule, lakini cha kushangaza ni kwamba huenda ratiba yao ya masomo ikavurugwa tena na kura ya maamuzi kwani shule ndizo hutumika kama vituo vya kupigia kura.

Mwaka huu unatupa fursa sisi kama nchi na serikali kutekeleza sera ambazo zitakuza maslahi na matakwa ya vijana. Tunahitaji serikali kuanzisha mikakati ili kuwasaidia walioathirika pakubwa na janga la korona.

Serikali inafaa kubuni mikakati mahsusi ili kukwamua sekta mbali mbali za kiuchumi ambazo ziiliathirik pakubwa kwa sababu ya janga la korona. Katika mikakati hii vijana wanafaa kupewa kipau mbele. Vijana ndio walioathrika pakubwa. Mikakati hii inahitaji kushirikisha wadau wote, kuanzia kwa vijana, kina mama , sekta ya elimu na sekta za kiuchumi. Viongozi wakilishi wa vijana katika bunge pia wanafaa kuwa katika mstari wa mbele kusukuma ajenda za vijana.

Tutaendelea kuishi kwa imani kwamba  tutakuwa na muamko mpya na hali zetu kuimarika, tutaendelea ‘kuvumilia kuwa Wakenya” tukipambana na hali zetu.

Ni wito wangu kwa viongozi wetu kwamba waweke kando siasa za kila mara na kwa mara ya kwanza waweke maslahi ya wananchi mbele  ili wazibe ufa badala ya kusubiri na kulazimika kujenga ukuta.  

Mwaka mpya mwanzo mpya, lakini changamoto bado ni zile zile, tushikane mikono tuimarishe nchi yetu.

Mhariri: Davis Ojiambo..