'Kuchoma vitu vya wanangu hakukumaliza majonzi, haki tu yaweza,' Mama ya ndugu waliouawa Kitengela azungumza

Ndugu ya Wanjiru, Joseph Macharia amesema kuwa dadake hajaweza kuzuia machozi kumdondoka tangu msiba huo kutokea.

Muhtasari

•Lucy Wanjiru alichoma hata michoro iliyokuwa imetengenezwa na mwanawe Fredrick Muriithi (30) aliyekuwa mchoraji pamoja na kanda na  karatasi za mwanawe Victor Mwangi (25) aliyekuwa  fundi na mcheza santuri.

•Fred alikuwa amechora michoro mingi ya familia yao; yeye, mama yake na ndugu yake pamoja. Licha ya pingamizi, Bi. Wanjiru alichoma michoro na picha hizo zote.

Lucy Wanjiru, Mama ya marehemu Fred Mureithi na Victor Mwangi
Lucy Wanjiru, Mama ya marehemu Fred Mureithi na Victor Mwangi
Image: MARGARET WANJIRU

Mama ya ndugu wawili ambao ni miongoni mwa vijana wanne waliouliwa na kikundi cha wafugaji wiki chache zilizopita maeneo ya Kitegela alichoma vitu vyao akitumai kuwa hatua hiyo ingemsaidia kupambana na majonzi na hasira aliyojawa nayo.

Lucy Wanjiru alichoma hata michoro iliyokuwa imetengenezwa na mwanawe Fredrick Muriithi (30) aliyekuwa mchoraji pamoja na kanda na  karatasi za mwanawe Victor Mwangi (25) aliyekuwa  fundi na mcheza santuri.

Hata hivyo, juhudi hizo zote alizofanyia katika lango la jumba lake lililo maeneo ya Syokimau kaunti ya Machakos hazikusaidia.

"Kuchoma vitu vya watoto wangu Fred na Victor hakukusaidia kumaliza majonzi, haki tu ndio yaweza kufanya hivo" Lucy alisema akiwa kwenye mahojiano na The Star.

Alirudi nchini kutoka Uingereza takriban wiki mbili zilizopita alipopata taarifa kuhusu mauji ya wanawe wawili yaliyofanyika mnamo Agosti 7.

Fred na Victor walikuwa miongoni mwa vijana wanne waliopigwa na kudungwa kwa mishale hadi kifo walipotuhumiwa kuwa wezi wa mifugo na baadhi ya wakazi wa Kitengela. Mali yao ikiwemo pikipiki tatu pia zilichomwa. Wengine walikuwa Mike George (29) na Nicholus Musa (28).

Ndugu ya Wanjiru, Joseph Macharia amesema kuwa dadake hajaweza kuzuia machozi kumdondoka tangu msiba huo kutokea.

"Mama yao haachi kulia. Anapoona chochote ambacho kinampatia kumbukumbu za wanawe anadondokwa na machozi" Macharia alisema.

Fred alikuwa amechora michoro mingi ya familia yao; yeye, mama yake na ndugu yake pamoja. Licha ya pingamizi, Bi. Wanjiru alichoma michoro na picha hizo zote.

"Huwezi kumaliza kumbukumbu za wanao ukichoma nyumba yote. Huwezi kuzuia uchungu wa mama aliyepoteza watoto wake wa pekee kwa namna ya unyama kama ile" Wanjiru alisema.

Haki tu ndiyo inaweza kunituliza. Haki tu itafanya nihisi vyema." Aliendelea kusema.

Alikuwa amezungumza na Fred siku mbili tu kabla ya mauti yake akimkumbusha kuhusu mkutano wake na mhubiri uliokuwa ufanyike siku ya Jumatano.

"Fred aliniambia kuwa hangehudhuria sherehe ya Victor kwani alikuwa na shughuli. Victor hakuwa na simu kwa hivyo tulizungumza kupitia simu ya ndugu yake" Bi Wanjiru alisema.

Baada ya kushindwa kupata wanawe kwa simu, Wanjiru ambaye ni mfanyibiashara Uingereza alipigia marafiki wake na majirani akiwauliza kuhusu wanawe.

"Jirani mmoja alinipigia siku mbili baadae akilia na kuniambia kuwa Freddie na Victor walikuwa wameuawa" Alisema.

Familia ya marehemu Fred na Victor inaomba haki itendeke haraka kuona kuwa siku 17 baadae ni mshukiwa mmoja tu amekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Wapelelezi wanachunguza ripoti kuwa takriban watu 500 maeneo ya Kitengela walikula kiapo kuficha majina ya waliohusika kwenye mauaji hayo.

(Utafsiri: Samuel Maina)