Majonzi ya mama! Mama ya ndugu walioliwa Kitengela azungumza baada ya kuwasili nchini kuzika wanawe

Familia na marafiki ambao walijumuika kumlaki uwanjani wa ndege walimfariji Wanjiru ambaye aliangua kilio baada ya kulemewa na hisia za majonzi.

Muhtasari

•Lucy Wanjiru ambaye ni mama wa Fredrick Mureithi na Victor Mwangi alitua nchini Jumapili asubuhi ili kuzika wanawe ambao walishambuliwa na kuuliwa usiku wa Jumapili iliyopita walipokuwa wametembea maeneo ya Kitengela.

•Bi Wanjiru alionekana kulemewa na majonzi alipokuwa anapelekwa kwa gari lililokuwa limeubiri kumpeleka nyumbani kwake Syokimau, kaunti ya Machakos.

Fredrick Muriithi, mama yake na ndugu yake mmdogo Victor Mwangi kwenye picha ya kitambo
Fredrick Muriithi, mama yake na ndugu yake mmdogo Victor Mwangi kwenye picha ya kitambo
Image: KURGAT MARINDANY

Mama wa ndugu wa wawili ambao walipoteza maisha yao pamoja na binamu wao wawili mikononi mwa wafugaji waliowashuku kuwa wezi wa mifugo amewasili nchini kutoka  Uingereza.

Lucy Wanjiru ambaye ni mama wa Fredrick Mureithi na Victor Mwangi alitua nchini Jumapili asubuhi ili kuzika wanawe ambao walishambuliwa na kuuliwa usiku wa Jumapili iliyopita walipokuwa wametembea maeneo ya Kitengela.

Familia na marafiki ambao walijumuika kumlaki  uwanjani wa ndege  walimfariji Wanjiru ambaye aliangua kilio baada ya kulemewa na hisia za majonzi.

"Nimefanya nini kustahili haya? Nimekukosea vipi Mungu kustahili kupoteza watoto wangu wapendwa?" Wanjiru ambaye aliyeonekana mwenye kuvunjika moyo alisema.

Bi Wanjiru alionekana kulemewa na majonzi alipokuwa anapelekwa kwa gari lililokuwa limeubiri kumpeleka nyumbani kwake Syokimau, kaunti ya Machakos.

Hata hivyo mama huyo ambaye hajaolewa aliambia ndugu yake Joseph Macharia kuwa hangeenda kwake kwani mazingira yale yangempatia  kumbukumbu za wanawe.

Alipelekwa mahali kwingine kupumzika kabla ya kupelekwa katika mochari ya hospitali ya chuo kikuu cha Kenyatta ambako miili ya wanawe imehifadhiwa.

Macharia alisema kuwa mazishi ya wawili hao ingefanyika siku ya  Ijumaa ama Jumamosi maeneo ya Leshau Pondo, Nyahururu.

Polisi wamesema kuwa uchunguzi bado unaendelea ingawa hakuna yeyote aliyekamatwa kufikia sasa.

(Utafsiri: Samuel Maina)