Kilio cha haki! Vijana 4 wa familia moja wauliwa na wafugaji waliowashuku kuwa wezi wa mifugo Kitengela

Inaripotiwa kuwa mama ya ndugu wawili waliofariki alipatwa na mshangao mkubwa baada ya kupokea habari hizo za kusikitisha na amekuwa hospitalini tangu afahamishwe.

Muhtasari

•Ndugu wawili na binamu wawili walikuwa wamehudhuria sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya jamaa wao wakati walipoteza maisha yao mikononi mwa wakazi wa maeneo ya Enkamulyat.

•Marafiki wa karibu walisema kuwa wanne hao walitumia  pikipiki tatu kuenda Kitengela. Baada ya kufika pale walienda kwa dada ya George ambaye aliwakaribisha.

•Kamanda wa polisi maeneo ya Kitengela Muthuri Mwongera alisema kuwa wanne hao walishambuliwa vibaya Jumapili jioni baada ya kutuhumiwa kuwa wezi wa mifugo.

Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Mike George 29, Fredrick Mureithi 22, Victor Mwangi 26, Nicholas Musa 28 na pikipiki zao zilizochomwa Kitengela
Image: KURGAT MARINDANY

Habari na Kurgat Marindany

Wanaume wanne kutoka familia moja wenye umri wa ujana walikumbana na kifo cha kusikitisha  usiku wa Jumapili baada yao kushukiwa kuwa wezi wa mifugo.

Ndugu wawili na binamu wawili walikuwa wamehudhuria sherehe ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya jamaa wao wakati walipoteza maisha yao mikononi mwa wakazi wa maeneo ya Enkamulyat.

Fred Mureithi (30), ndugu yake mdogo Victor Mwangi  ambaye alikuwa anaadhimisha kuhitimu miaka 25 na binamu wao Mike George (29) na Nicholas Musa (28)  walichukua pikipiki zao kuenda kununua kuku maeneo ya Kisaju bila kujua kifo kilikuwa kinawabishia hodi.

Waliamua kusimama  kando ya mto ulio maeneo ya Enkamulyat na wafugaji ambao waliona pikipiki zikiwa zimeegeshwa kando ya mto wakashuku kuwa wenye pikipiki zile walikuwa kwenye harakati ya kuiba mifugo.

Bila kuwa nafasi ya kujitetea wafugaji wale waliwashambulia vijana hao kwa kutumia mikuki hadi wakaaga kisha wakachoma pikipiki zao.

Marafiki wa karibu wamesema kuwa wanne hao walitumia  pikipiki tatu kuenda Kitengela. Baada ya kufika pale walienda kwa dada ya George ambaye aliwakaribisha.

Walipokuwa pale waliamua kula kuku kama chakula cha jioni na hapo ndipo wakachukua pikipiki zao na kuenda kutafuata kuku wa kupika.

Kamanda wa polisi maeneo ya Kitengela Muthuri Mwongera alisema kuwa wanne hao walishambuliwa vibaya Jumapili jioni baada ya kutuhumiwa kuwa wezi wa mifugo.

Mwongera alisema kuwa kesi za wizi wa mifugo ni nyingi katika eneo ambapo marehemu walikumbana na kifo chao ila akasema kuwa hali hiyo haikufaa kuwafanya wakazi kuchukua uamuzi huo.

Wanafamilia wamesema kuwa mama ya ndugu wawili waliofariki alipatwa na mshangao mkubwa baada ya kupokea habari hizo za kusikitisha na amekuwa hospitalini tangu afahamishwe.

Miili ya wanne hao imehifadhiwa katika mochari ya jiji la Nairobi.

Wanamitandao waliojawa na ghadhabu wameendelea kutoa shinikizo kwa maafisa wa usalama kuchukua hatua ya haraka kuhakikisha haki imepatikana.

Baadhi yao wanadai kuwa huenda nywele za rasta ambazo marehemu walikuwa nazo kichwani zilifanya wauaji wao wawashuku kuwa wezi.