Zaidi ya wanawake watano huuawa kila saa na mwanafamilia- UN

Afrika ni eneo la pili baada ya Asia, kurekodi visa vya mauaji ya wenzi wa karibu wa kike/familia, vikiwa 17,200.

Muhtasari

• Maadhimisho ya kimataifa ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaanza Ijumaa, chini ya kaulimbiu, ‘Ungana! Harakati za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.’

afrimax
afrimax

Karibu wanawake na wasichana 45,000 duniani waliuawa na wapenzi wa karibu au wanafamilia mwaka 2021 kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa.

Hii ina maana kwamba zaidi ya wanawake au wasichana watano wanauawa kila saa na mtu katika familia zao.

Ingawa idadi hii ni ya kushangaza, ripoti iliyotolewa kwa pamoja na ofisi ya Umoja wa Mataifa kuhusu madawa ya kulevya na uhalifu (UNODC) na wanawake wa Umoja wa Mataifa, ilifichua kwamba kiwango cha kweli cha mauaji ya wanawake kinaweza kuwa kikubwa zaidi.

Afrika ni eneo la pili baada ya Asia, kurekodi visa vya mauaji ya wenzi wa karibu wa kike/familia, vikiwa 17,200.

Hata hivyo, bara hilo linachukuliwa kuwa eneo lenye kiwango cha juu cha unyanyasaji, ikilinganishwa na ukubwa wa idadi ya wanawake.

"Wanawake na wasichana wa Afrika wako katika hatari kubwa ya kuuawa na wapenzi wao wa karibu au wanafamilia wengine."

Upungufu wa data umeonekana kuwa changamoto, kwani kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kati ya mauaji ya wanawake 81,000 yanayokadiriwa mwaka 2021, wanne kati ya kumi, hawana ‘taarifa za muktadha’ kuruhusu kutambuliwa na kuchukuliwa kuwa mauaji yanayohusiana na jinsia.

"Takwimu kuhusu mauaji yanayohusiana na jinsia yanayofanywa katika nyanja ya umma ni chache sana, na hivyo kufanya kuwa vigumu kujulisha sera za kuzuia mauaji ya aina hii."

Umoja wa Mataifa unatoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya ulinzi kwa wanawake watetezi wa haki za binadamu na wanaharakati wa haki za wanawake.

"Natoa wito kwa serikali na washirika kote duniani kuongeza ufadhili wa muda mrefu na msaada kwa mashirika ya haki za wanawake."

Mkurugenzi mtendaji wa UN Women Sima Bahous alisema.

Haya yanajiri huku maadhimisho ya kimataifa ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yakianza Ijumaa, chini ya kaulimbiu, ‘Ungana! Harakati za kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.’