Kila kitu unafaa kujua kuhusu Mashujaa Dei na kwa nini huadhimishwa Oktoba 20 kila mwaka

Kuzuiliwa kwa Kapenguria Six mwaka 1952 kunachukuliwa kuwa tukio maarufu kwa hivyo kuadhimishwa kwake na likizo ya umma mnamo Oktoba 20 kila mwaka.

Muhtasari

• Baada ya uhuru, Jomo Kenyatta aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kenya kuanzia 1963 hadi 1964.

• Baadaye, akawa rais wa kwanza wa Kenya kuanzia 1964 hadi 1978, alipoaga dunia.

 

Mashujaa Day
Mashujaa Day
Image: The Star

Ijumaa hii, Oktoba 2o itakuwa sikukuu kubwa sana nchini Kenya, na sherehe zitaandaliwa katika kaunti ya Kericho zikiongozwa na rais William Ruto.

Sikukuu hiyo inakwenda kwa jina Mashujaa Dei. Lakini je, ni nini dhima ya siku hii?

Siku hiyo huadhimishwa tarehe 20 Oktoba kila mwaka ili kuwakumbuka mashujaa wakuu wa nchi. Hata hivyo, ingawa imetengwa kwa ajili ya kuwaenzi na kuwakumbuka mashujaa wa nchi hii waliopigania uhuru wake kutoka kwa utawala wa kikoloni, siku hiyo inawakilisha mengi zaidi ya inavyoonekana.

Inaadhimishwa kama njia ya kuwaheshimu kwa pamoja watu waliochangia pakubwa katika harakati za kupigania uhuru wa Kenya. Aidha, pia walitoa michango chanya kwa nchi hiyo baada ya uhuru.

Hapo awali, likizo hiyo ilijulikana kama Siku ya Kenyatta. Hii ni kwa sababu ilipewa jina la Jomo Kenyatta – aliyekuwa kinara wa vuguvugu la Mau Mau na mwanaharakati wa kupinga ukoloni wa Kenya na mwanasiasa.

Baada ya uhuru, Jomo Kenyatta aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Kenya kuanzia 1963 hadi 1964. Baadaye, akawa rais wa kwanza wa Kenya kuanzia 1964 hadi 1978, alipoaga dunia.

Wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Kenya kutoka kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza, Jomo Kenyatta alijitokeza kama mmoja wa wapiga kampeni mashuhuri. Mnamo Oktoba 1952, alikamatwa pamoja na wapigania uhuru wengine watano wa Kenya.

Sita hao walikamatwa kwa madai ya kuwa wanachama wa Mau Mau. Uasi wa Mau Mau ulikuwa ni vuguvugu lililowaasi watawala wa Uingereza wa Kenya. Kundi la washtakiwa sita lilijulikana kama Kapenguria Six. Mbali na Jomo Kenyatta, wengine watano walikuwa:

1.Achieng Oneko Ramogi

Achieng Oneko alikuwa mwanasiasa wa Kenya na mpigania uhuru aliyechukuliwa kuwa shujaa wa taifa. Kwa mujibu wa vitabu na Makala ya kihistoria, Oneko alizaliwa mwaka wa 1920 katika kijiji cha Tieng'a katika eneo dogo la Uyoma katika Wilaya ya Bondo na alifariki mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 87.

2. Bildad Kaggia

Kaggia alikuwa mwanasiasa wa Kenya, mwanaharakati na mzalendo. Alikuwa mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ya Mau Mau. Baada ya utawala wa kikoloni, Bildadi akawa Mbunge. Alitambuliwa kama mwanajeshi na mzalendo mkali. Ajenda kuu ya Bildadi ilikuwa kuwahudumia watu masikini na wasio na ardhi nchini Kenya. Kwa sababu hii, alikuwa na mzozo usioweza kusuluhishwa na Rais Jomo Kenyatta. Alifariki tarehe 7 Machi 2005 akiwa na umri wa miaka 84.

3. Fred Kubai

Fred Kubai alikuwa mmoja wa wanachama sita wa Kapenguria wa Muungano wa Afrika wa Kenya ambao walikamatwa, kuhukumiwa, na kufungwa mwaka wa 1952. Alipanga mashambulizi dhidi ya serikali ya Ulaya huko Nairobi. Alikuwa kiongozi wa Muungano wa Uchukuzi wa Wafanyakazi wa Kenya na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi wa Afrika Mashariki. Kubai alifariki tarehe 1 Juni 1996 akiwa na umri wa miaka 79 kwa mujibu wa historia.

4. Kung’u Karumba

Kung’u Karumba alikuwa mzalendo na mpigania uhuru wa Kenya. Baada ya Kenya kupata uhuru, Kung’u alisalia kuwa marafiki wazuri na Jomo Kenyatta. Pia akawa mshauri mwenye ushawishi kwake. Pia alikuwa mfanyabiashara mahiri na uwekezaji mkubwa nchini Uganda. Alifariki mwaka wa 1978 akiwa na umri wa miaka 76.

5. Paul Ngei

Ngei alikuwa mwanasiasa wa Kenya na mmoja wa Kapenguria Six. Baada ya Kenya kupata uhuru, alishikilia nyadhifa kadhaa za uwaziri serikalini. Paul Ngei alifariki tarehe 15 Agosti 2004 akiwa na umri wa miaka 80.

Kuzuiliwa kwa Kapenguria Six kunachukuliwa kuwa tukio maarufu kwa hivyo kuadhimishwa kwake na likizo ya umma mnamo Oktoba 20 kila mwaka.

Likizo ya umma iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mnamo 1958, haswa na wanaharakati lakini ilipata mafanikio zaidi mwaka uliofuata. B

aada ya uhuru mwaka wa 1963, sikukuu hiyo iliwekwa katika katiba ya Kenya kama Siku ya Kenyatta. Hata hivyo, mnamo Agosti 2010, baada ya kupitishwa kwa katiba mpya, mabadiliko kadhaa yalifanywa kwa sikukuu za umma. Kwa hiyo, Siku ya Kenyatta ilibadilishwa jina. Siku hiyo tangu wakati huo imepanua wigo wake na kujumuisha mashujaa wengi wa Mashujaa Day.