Baada ya kuhudumu kwa miezi 11 tu, kikosi cha Afrika Mashariki kilichoundwa ili kukabiliana na ghasia za wanamgambo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kimeamriwa kuondoka.
Serikali ya Congo ilisema haitaongeza muda wa Jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya miezi kadhaa ya Kinshasa kulalamikia kutofanya kazi kwa vikosi hivyo.
Uamuzi wa kutoongeza muda wa wanajeshi hao unakuja huku ghasia kati ya kundi la waasi la M23 na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali zikizuka katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mara nyingine tena.
Je, jukumu la kikosi cha kikanda lilikuwa lipi?
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) - muungano wa nchi saba - ilituma wanajeshi wake DR Congo mwaka jana baada ya mapigano kuzuka upya kati ya majeshi ya serikali na waasi wa kundi la M23. Kikosi hicho kilikubaliwa muda mfupi baada ya DR Congo kujiunga na Jumuiya hiyo.
Kundi la M23 lililoundwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, limechukua udhibiti wa maeneo makubwa ya eneo la mashariki, likisema kwamba linafanya hivyo ili kutetea maslahi ya jamii ya Watutsi dhidi ya wanamgambo wa Kihutu ambao linasema wanaungwa mkono na serikali.
Burundi ilikuwa nchi ya kwanza kati ya nchi nne kutuma wanajeshi wake nchini DR Congo Agosti mwaka jana, ikifuatiwa na Kenya, Sudan Kusini na Uganda, huku Kenya ikiwa na kamandi ya jumla.
Jeshi la Kanda la EAC linasisitiza kuwa jukumu lake ni kusimamia uondoaji wa makundi yenye silaha kutoka maeneo yaliyotekwa.
Hata hivyo, serikali ya Congo na jumuiya za wenyeji wanataka jeshi hilo lishiriki katika mapambano ya moja kwa moja dhidi ya makundi kama vile M23.
Kikosi hicho kilianzishwa kufanya kazi pamoja na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa ambao tayari walikuwa nchini humo. Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, kinachojulikana kama Monusco, kimezidi kupoteza umaarufu kwa kushindwa kumaliza mzozo huo licha ya kuhudumu nchini humo kwa miaka 25. Rais Félix Tshisekedi alisema alianataka Monusco kujiondoa nchini humo mwezi Disemba.
Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Jumuiya ya Afrika Mashariki ilisema vikosi vyake vimejitolea kufanya kazi kwa karibu na serikali ili kuwezesha wakimbizi wa ndani kurejea katika makazi yao wakiwa salama na kuimarisha ulinzi wa raia kwa ujumla.
Mamlaka yake yameongezwa mara mbili tangu misheni hiyo ilipoanza.
Kwa nini DR Congo inataka wanajeshi wa Afrika Mashariki waondoke?
Kikosi cha EAC kimekuwa kikikosolewa mara na serikali ya Congo na mashirika ya kiraia tangu kilipowasili nchini humo.
Rais Tshisekedi amekuwa mmoja wa wakosoaji wakuu wa kikosi hicho. Amelalamika kuhusu "ukosefu wa ufanisi" wa ujumbe huo, akitaka kichukue hatua kali zaidi dhidi ya M23 au kuondoka nchini.
Kushindwa kumaliza mzozo huo kumesababisha maandamano dhidi ya vikosi vya EAC na Monusco. Maandamano ya aina hiyo mwezi Septemba yaligeuka kuwa ghasia, baada ya zaidi ya watu 40 kupoteza maisha.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, Waziri wa Mawasiliano Patrick Muyaya alisema: "Ujumbe uko wazi: Jeshi la kikanda la EAC lazima liondoke Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ifikapo tarehe 8 Desemba, kama ilivyokubaliwa, kwa sababu haijaweza kutatua tatizo, hasa lile la M23."
Je, kikosi cha EAC kimepata mafanikio gani?
Tangu kuingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka jana, jeshi la EAC lilisema limemamia uondoaji wa makundi yenye silaha kutoka maeneo kadhaa kama Karuba, Mushaki, Kiloriwe na Kitchange.
Hata hivyo, haijafikia uthabiti kamili wa maeneo hayo kutokana na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na matatizo ya vifaa na uendeshaji.
Siku ya Jumanne, mwanajeshi wa Kenya aliuawa katika shambulio la waasi. Alikuwa mwanajeshi wa kwanza wa Kenya kuuawa.
Mapema mwezi huu EAC ilisema vikosi vyake vimekabiliwa na uhasama kwa sababu ya propaganda zinazoendelezwa na makundi yenye silaha.
Kwanini mapigano yamezuka tena?
Makumi ya makundi yenye silaha kwa muda mrefu yamekuwa yakidhibiti eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Baada ya mkataba wa kusitisha vita kufikiwa kwa miezi sita, mapigano yalianza tena kati ya waasi wa M23 na vikosi vinavyounga mkono serikali, vinavyojulikana kama Wazalendo, mwezi huu.
Serikali ya Kinshasa ilishutumu M23 kwa kukataa kuweka chini silaha na kuzingatia makubaliano ya kusitisha mapigano. Kundi la M23 kwa upande wake lililaumu vikosi vinavyounga mkono serikali kwa kuanzisha tena ghasia hizo.
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilisema bado linaheshimu Makubaliano ya kisitisha vita, lakini mashahidi wanapinga hilo, wakisema wanajeshi na makundi yanayoiunga mkono serikali yamekuwa yakishirikiana kukipigana dhidi ya M23.
Raia wamenaswa katika ghasia mpya - wiki iliyopita karibu watu 60 waliuawa katika mashambulizi katika eneo la Rutshuru Kivu Kaskazini, afisa wa eneo hilo alisema.