Saa kadhaa kabla ya maandamano ya kitaifa Kenya dhidi ya kuongezeka visa vya mauaji na unyanyasaji wa wanawake – kanda ya video ilichapishwa katika mtandao wa kijamii ilioonyesha jinsi chuki dhidi ya wanawake ilivyokithiri nchini.
Katika sehemu moja ya mji mkuu Nairobi ambapo baadhi ya wanawake walikusanyika kwa maandamano hayo mwishoni mwa juma lililopita, wanaume wawili walirekodiwa kwa kamera wakiteta kuhusu kwanini maandamano hayo yanafanyika.
"Wanaume wameteseka kwasababu ya wanawake," mmoja analalamika akiendelea kusema kwa mtazamo wake wanawake wanawatumia wanaume kwa ajili ya pesa zao.
Wakati mazungumzo hayo makali yakiendelea, mwenzake anaingilia na wanaanza kunyoosha kidole kwa kamera na kuwapigia wanawake kelele: "Tutawaua."
Kanda hiyo ilisambazwa mtandaoni na mwanaharakati Boniface Mwangi huku akiambatanisha ujumbe: "Mimi kama mwanamume na baba, wanaume hawa hawawawakilishi wanaume ninaowatambua."
Lakini tatizo kama anavyoeleza ni kwamba ni wanaume wachache wanaojitokeza nchini kuzungumza dhidi ya kauli kama hizi.
" Sisi kama wanaume wa Kenya tunapaswa kuzungumza kwa nguvu na kwa ujasiri," alisema kuhusu mauaji ya wanawake ambao wanauawa kwasababu ya jinsi yao.
Ni kauli ambayo Felix Kiprono, afisa wa habari katika kampuni ya uchambuzi wa data Odipo Dev.
Yeye pamoja na wenzake hivi karibuni walichapisha ripoti kuhusu mauaji yanayoongezeka kwa kasi nchini Kenya ya wanawake - takriban visa kumi vimeripotiwa katika mwezi wa kwanza wa mwaka huu pekee vya mauaji ya wanawake.
Kisa kimoja cha mauaji mabaya, ni kuhusu muathiriwa aliyekatwa katwa na baadhi ya sehemu za mwili zikapatikana zimetiwa ndani ya fuko wa plastiki na kufichwa katika nyumba ya kukodi.
Ripoti hiyo iliopewa jina ‘Silencing Women’, "imenuia kuangazia ukweli wa maisha ya wanawake yalio katika hatari, na kutoa taarifa muhimu kukabiliana na visa vya waathiriwa kulaumiwa, visa kutorepotiwa ipasavyo na kushinikiza hatua kuchukuliwa".
Lakini Kiprono ameshangazwa na ripoti ilivyopokewa, hususan katika mitandao ya kijamii, ambayo mara nyingine inatambulika kama sehemu ya wanaume na ilio na chuki dhidi ya wanawake – mtandao wa majukwaa inayohimiza mfumo dume na kuwapinga wanawake.
Ameiambia BBC kwamba shutuma zimedhihirika kote: "Sio Twitter lakini pia kwenye TikTok, ambalo huwa ni jukwaa salama."
Huku ripoti hiyo sasa ikiwa hadharani, yeye na wenzake sasa wamekuwa wakipokea maombi mengi ya kutaka kuhojiwa.
"Inaonekana kuwa ni vigumu kuwapata wanaume kulizungumzia suala hili wazi," anasema.
Jambo jingine linalojitokeza kwenye hisia ni kuwa wanaume hawajaonyesha hamu kuhusika katika mijadala katika mitandao kuhusu mambo yanayojitokeza kwenye ripoti hiyo.
"Tulipokuwa tukitathmini data, tuligundua, sana sana katika Instagram na TikTok, kuwa takriban 90% ya wanaochangia ni wanawake," Kiprono amesema.
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wanawake UN Women, data kuanzia 2022 imeonyesha kuwa "Afrika ilinakili kiwango kikubwa cha mauaji ya wanawake kilichotekelezwa na mpenzi au jamaa ya muathiriwa katika visa vya wanaokadiriwa kuwa waathirirwa 20,000".
Afrika inafuatwa nyuma na "18,400 barani Asia, 7,900 Amerika, 2,300 Ulaya na 200 huko barani Oceania".