logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Wanawake 6 walioweka historia ya kutalii anga za mbali

Ni kwa mara ya kwanza katika miaka zaidi ya 60, wanawake pekee wanasafiri kwenda anga za mbali bila kujumuika na mwanaume.

image
na Davis Ojiambo

Makala15 April 2025 - 15:23

Muhtasari


  • Safari hiyo ya kihistoria ilidumu kwa dakika 11 pekee lakini ilibeba maana kubwa zaidi ya muda huo mfupi. 
  • Wanawake hao walivuka mpaka wa anga unaotambulika kimataifa mstari wa Kármán 
  • Chombo kilitua taratibu kwa msaada wa parachuti katika jangwa la Texas.

Wanawake 6 walioweka historia ya kutalii anga za mbali

Katika tukio la kihistoria lililotikisa dunia, roketi ya New Shepard inayomilikiwa na kampuni ya Blue Origin ya Jeff Bezos ilirushwa kutoka Texas, Marekani, ikiwa imebeba wanawake sita waliounda kundi la kwanza la wanawake pekee kufika angani tangu mwaka 1963.

Ni kwa mara ya kwanza katika miaka zaidi ya 60, wanawake pekee wanasafiri kwenda anga za mbali bila kujumuika na mwanaume.

Safari hiyo ya kihistoria ilidumu kwa dakika 11 pekee lakini ilibeba maana kubwa zaidi ya muda huo mfupi. Wanawake hao walivuka mpaka wa anga unaotambulika kimataifa mstari wa Kármán na kurudi salama duniani huku wakiweka alama ya milele katika historia ya safari za anga.

Mwanamuziki Katy Perry alijiunga na mpenzi wa mfanyabiashara Jeff Bezos, Lauren Sanchez, mtangazaji wa televisheni ya CBS Gale King, mwanasayansi wa makombora wa NASA Aisha Bowe, mwanaharakati wa haki za binadamu Amanda Inguen, na mtayarishaji wa filamu Garrett Flynn.

Roketi ilirushwa kwa kasi na ndani ya dakika saba, ambapo chombo cha anga kilitenganishwa na roketi na kutupwa angani kama jiwe linavyotupwa juu, chombo hicho kikavuka mpaka wa anga na kuwapa wanawake hao hisia ya kutokuwa na uzito wakiwa juu ya mstari wa Kármán, takribani kilomita 100 kutoka usawa wa bahari.

Chombo hicho kilikuwa kinajiendesha chenyewe, kisichohitaji rubani wala uendeshaji kutoka kwa abiria. Baada ya muda mfupi wa kuangalia uzuri wa Dunia kutoka juu na kupata uzoefu wa na hisia za kipekee kama kundi la wanawake walioandika historia, chombo kilianza safari ya kurudi duniani.

caption

Blue Origin imefanya safari nyingi kama hii lakini hii ilikuwa maalum. Lengo la Safari hii ilikuwa ni kuhamasisha utalii wa anga. Na wenyewe wanasema lengo si tu kukuza sekta ya utalii wa anga, bali pia kuvunjilia mbali mitazamo ya kijinsia, kuonyesha kuwa wanawake nao wana nafasi katika maeneo ya juu kabisa ya mafanikio ya kibinadamu, ikiwemo hili la kusafiri anga za mbali, linaloonekana haliwezekani bila mwanaume

Kama ilivyoelezwa na Blue Origin: "Hii si misheni ya kawaida ya anga. Ni misheni ya kuhamasisha vizazi vijavyo."

Chombo kilitua taratibu kwa msaada wa parachuti katika jangwa la Texas. Wakati huo huo, chombo kilichokuwa kinaendesha roketi kilichokuwa kimewatuma huko angani kilitua chenyewe umbali wa kilomita chache kutoka eneo ambalo walianza safari.

Baada ya kutua, bilionea Jeff Bezos mwenyewe alikuwepo kuwakaribisha. Katy Perry na Gayle King waliibusu ardhi kwa furaha walipotoka kwenye chombo hicho, ishara ya kushukuru maisha na mafanikio hayo.

Wakati wa uzinduzi na kuanza kwa safari, familia na marafiki walikuwepo, akiwemo Oprah Winfrey, baadhi ya familia ya Kardashians, na kundi la wanawake wana anga. Machozi ya furaha yaliwatiririka wote walipoona chombo kimetua salama kutoka anga za mbali.

Kila mmoja wa wanawake hao alitoa maneno ya kugusa moyo baada ya tukio hilo na kutua salama duniani:

Gayle King - "Nilihitaji tu kuchukua muda na kuthamini ardhi."

Lauren Sánchez- "Kulikuwa na mshikamano wa ajabu kati yetu. Najivunia sana kikosi hiki."

Amanda Nguyen- "Nilijiapia kamwe sitakata tamaa. Leo nashukuru kwa safari hii ya kipekee."

Kerianne Flynn- "Rafiki wa mwanangu alimwambia 'Mama hawaendi angani'. Lakini mama huyu ameenda angani!"

Aisha Bowe- "Sitakuwa mtu yule yule tena. Kulikuwa na nishati ya kipekee ndani ya kapsuli."

Katy Perry- "Kwenda angani ni jambo la pili kwa umuhimu baada ya kuwa mama. Labda nitapiga wimbo kuhusu hili!"

Mstari wa Kármán ni nini?

Mstari wa Kármán ni mpaka wa kufikirika unaotambulika kimataifa kuwa ndio mwanzo wa anga ya juu na dunia, kilomita 100 kutoka usawa wa bahari.

Kulingana na Fédération Aéronautique Internationale, eneo hili linatenganisha anga ya Dunia na anga ya nje (astronomia).

Kwa mujibu wa Profesa T.V. Venkateswaran, asilimia 99.9 ya anga ya dunia ipo chini ya mstari huo, hivyo yeyote anayevuka mstari huo anachukuliwa kama msafiri wa anga za mbali.

Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved