Karua, ahoji umuhimu wa BBI na marekebisho ya katiba

Muhtasari

• Aliwataka wakenya kutounga mkono mapendekezo ya BBI kurekebisha katiba.

• Karua alisema Kenya haihitaji BBI kuendelea na kuwepo kwa ustawi na kushikilia kwamba katiba ya 2010 inatosha kustawisha taifa la Kenya.

Kiongozi wa NARC-Kenya Martha Karua
Kiongozi wa NARC-Kenya Martha Karua

Marekebisho ya katiba yanayoshinikizwa na rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga chini ya mchakato wa BBI ni haramu na hayafai kufanyika.

Kiongozi wa NARC Kenya Martha Karua siku ya Jumapili aliwataka wakenya kutounga mkono mapendekezo ya BBI kurekebisha katiba, mapendekezo ambayo alisema ni kinyume cha sheria na yameletwa wakati usiyofaa.

 “Acha Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wajue kuwa haturudi kwa udikteta. Hatutakubali damu, jasho na machozi ya Wakenya wengi mashujaa waliopigana na mwishowe kuangusha udikteta wa KANU kwenda bure – sio kama sisi tukishuhudia, ”Bi Karua alisema.

Karua ambaye alikuwa waziri wa sheria katika serikali ya rais msataafu Mwai Kibaki alisema kwamba rais Kenyatta na Raila wanafaa kuangazia janga la COVID-19 na kutafuta suluhu kwa changamoto zinazowakabili wananchi wa kawaida.

Karua alisema kwamba Kenya haihitaji BBI kuendelea na kuwepo kwa ustawi na kushikilia kwamba katiba ya 2010 inatosha kustawisha taifa la Kenya.

Mbunge huyo wa zamani wa Gichugu alisema kwamba wakenya wanakabiliwa na changamoto nyingi zilizotokana na janga la korona kama vile ukosefu wa ajira  na kutokuwepo kwa matumaini.

Alipuuzilia mbali madai ya wanaoshinikiza BBI kuwa Kenya kwa sasa inakabiliwa na muda wa kikatiba na kwamba wanafaa kukubali marebisho yanayopendekezwa katika BBI.

Karua alikosoa ushirikiano baina ya rais Kenyatta na Raila Odinga akisema kwamba umesambaratisha upinzani na kuipa serikali uhuru wa kufanya kile inataka bila mtu wa kuwauliza maswali. Alisema kwa sasa Kenya haina upinzani.