Msimamo wa Ruto kuhusu BBI waacha wandani wake kwa njia panda

Muhtasari

•Oparanya akaribisha hatua ya Ruto kuunga mkono BBI

•Mwangi kiunjuri kuunga mkono BBI 

• Kiunjuri asema kwamba BBI sasa imezingatia matakwa ya wananchi

Naibu rais William Ruto.
Naibu rais William Ruto.

Baada ya naibu rais William Ruto kuonyesha ishara za kubadili msimamo wake kupinga mchakato wa BBI viongozi wengi wanaoegemea mrengo wake na  ambao walikuwa wakipinga BBI wanaendelea kubadili misimao yao na kuanza kuunga mkono mabadiliko hayo ya katiba yanayoendeshwa na rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wa hivi punde kutangaza kuunga mkono BBI ni aliyekuwa waziri wa kilimo Mwangi Kiunjuri ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa mchakato wa BBI na “handshake”.

Kiunjuri siku ya Jumamosi alisema kwamba ripoti ya BBI iliyofanyiwa marekebisho ina timiza matakwa yake na baadhi ya viongozi waliokuwa wakiipinga na sasa hana budi kuiunga mkono.

Alisema kwamba atakutana na baadhi ya viongozi kujadili ripoti hiyo kwa kina, huku akisema kwamba katika ripoti hiyo Kaunti ya Laikipia itapata eneo bunge moja zaidi ambayo ni habari njema kwa wenyeji.

Kwingineko, Mwenyekiti wa baraza la magavana ambaye pia ni gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya amekaribisha hatua ya naibu rais William Ruto kubadili msimamo wake kuhusu BBI.

Oparanya alimtaka Ruto sasa kujiunga na viongozi wenzake kupigia dembe ripoti ya BBI na kuwataka viongozi wengine waliokuwa wakieneza uongo dhidi ya BBI kushirikana na wenzao kufanikisha ripoti hiyo.

Aliwawahakikishia wananachi wa kaunti ya kakamega kwamba BBI ina mapendekezo mazuri yatakayonufaisha wananchi wa kawaida.