Hofu Nakuru baada mwanamke kupatikana ameuawa huku damu ikidondoka kwenye sehemu zake za siri

Marehemu alikuwa na watoto wawili, mmoja wa miaka kumi na mwingine wa miezi minne wote ambao walikuwa pale ndani ya nyumba wakati wa mauaji hayo.

Muhtasari

•Moses Leparani (35) anatuhumiwa kuua Martha Waithera  (33) nyumbani kwake maeneo ya Lake View, Nakuru usiku wa kuamkia Jumanne.

•Kulingana na naibu kamishna wa polisi maeneo ya Nakuru Mashariki Eric Wanyonyi, mwili wa Waithera  ulikuwa na ishara za kudhulumiwa ikiwemo damu iliyokuwa kwenye sehemu zake za siri.

Marehemu Martha Waithera na mpenzi wake Moses Leparani
Marehemu Martha Waithera na mpenzi wake Moses Leparani
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ya Nakuru wanawinda mwanaume mmoja anayedaiwa kuua mpenzi wake kisha kuenda mafichoni.

Moses Leparani (35) anatuhumiwa kuua Martha Waithera  (33) nyumbani kwake maeneo ya Lake View, Nakuru usiku wa kuamkia Jumanne.

Jirani mmoja wa marehemu, Margaret Nyambura, ambaye pia ni binamu yake amesema kuwa alifahamishwa  kuhusu mauaji hayo na mtoto wa marehemu mwenye umri wa miaka kumi.

Nyambura amesema kuwa mshukiwa alihamia kwenye nyumba ya marehemu takriban miaka tatu iliyopita na wamekuwa wakiishi pamoja tangu wakati huo.

Alisema kuwa alishindwa kwenda kuthibitisha taarifa aliyopatiwa na mpwa wake na akafahamisha jirani mwingine ambaye aliingia ndani ya chumba kile na kuthibitisha.

"Mtoto aliniambia 'mama amekufa!'. Ndipo nikafungua mlango nikaanza kuita bwana ya marehemu. Mtoto akaniambia kuwa babake hayuko. Akaniambia niende niangalie, nikamwambia kuwa mimi sitaingia. Nikamwambia tutoke nje twende, nikafunga mlango nikaenda kuita mama mwingine wa ploti.Huyo mama ndiye alienda akafungua mlango akenda kwa kitanda akaniambia ni ukweli" Nyambura alisema.

Baada ya kuthibitisha hayo majirani walifahamisha chifu na maafisa wa polisi ambao walifika kwenye eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu.

Kulingana na naibu kamishna wa polisi maeneo ya Nakuru Mashariki Eric Wanyonyi, mwili wa Waithera  ulikuwa na ishara za kudhulumiwa ikiwemo damu iliyokuwa kwenye sehemu zake za siri.

"Tumeona kwamba mwili uko na majeraha na damu ilikuwa ikitokea kwenye sehemu zake za siri kumaanisha kuwa iko kitu kilifanyika kwake. Mwili umechukuliwa na upasuaji wa mauti utafanyiwa ili kubainisha kama mama aliuawa ama alikufa vipi" Bw Wanyonyi alisema.

Wanyonyi amesema kuwa mpenzi wa marehemu ndiye mshukiwa mkuu kwani kwa sasa hajulikani mahali alipo.

Marehemu alikuwa na watoto wawili, mmoja wa miaka kumi na mwingine wa miezi minne wote ambao walikuwa pale ndani ya nyumba wakati wa mauaji hayo.

Bw Wanyonyi ameshauri wanawake kuchunguza vizuri tabia za wanaume ambao wanakaribisha kuishi nao nyumbani kwao.

"Ningependa kushauri kina mama ambao wanataka kukaribisha wanaume waishi nao wajaribu sana kuchunguza tabia zao. Tumekuwa na wanaume wabaya sana ambao wanatesa wanawake mpaka sasa wanawaua. Ikiwa mtu anatoka mbali kuja kuishi na wewe jaribu sana kumchunguza." Wanyonyi alisema.