Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi siku ya Alhamisi alisema kwamba kisa cha hivi punde cha jengo kuporomka Ruaka ni cha nane katika kaunti ya kiambu kwa kipindi cha chini ya miezi sita.
Aliyataja maeneo kama Kasarani, Kinoo na Ruiru ambayo yameshuhudia visa vya hivi punde vya majengo kuporomoka.
Mbali na hayo Wamatangi alisema atamenyana na wamiliki wa nyumba ambao hawafuati sheria zilizowekwa na halmashauri ya ujenzi nchini NCA.
Kulingana na Gavana Kimani Wa Matangi agizo lilikuwa limetolewa kusitisha ujenzi wa jengo hilo ila wasimamizi walipuuzilia.
''Hilo jengo lilikuwa limepigwa marufuku tangu mwezi wa Mei 2022 na mara nyingi wameshikwa na maafisa wa polisi na wakiachiliwa wanarudi kwenye ujenzi'' Wamatangi alisema.
Aliahidi kuandaa kikao cha haraka na mamlaka ya kusimamia ujenzi NCI kujaribu kupata suluhu ya kudumu na kuhakikisha mtu yeyote anaye endeleza ujenzi bila idhini wala stakabathi zinazofaa achukuliwe hatua mara moja.'