Wamiliki wa Matatu na magari ya uchukuzi wa umma nchini sasa wanatoa wito kwa mamlaka ya usalama barabarani NTSA kuacha kutoa leseni za udereva.
Muungano huo wa wamiliki wa matatu wanasema kuwa utoaji wa leseni unafaa kuhamishwa kutoka NTSA hadi huduma ya vijana kwa kaifa NYS.
Chama hicho kimesema kwa kawaida NTSA hutoa hati muhimu kwa madereva ambao hawafikii kikomo cha kuendesha Magari ya Watumishi wa Umma.
"Sote tunajua kuwa NYS inasifika kwa kutoa madereva waliohitimu zaidi kutokana na kuwa na uwezo wa kupima na kuainisha madereva," mwenyekiti wa chama hicho, Bw Simon Kimutai alinukuliwa na jarida moja la humu nchini.
Bw Kimutai alikuwa akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Chama cha Wamiliki wa Matatu (MOA) na wanachama wa Chama cha Kitaifa cha Usalama Barabarani ambao pia ulihudhuriwa na wanachama wa Chama cha Magavana wa Mwendo Kasi.
Chama cha Wamiliki wa Matatu kilisema NTSA inafaa kulaumiwa kwa utoaji wa leseni ovyo. Alisema NTSA inafaa kuhakikisha madereva wanafanya mazoezi kabla ya kukabidhi leseni kwa yeyote anayetaka kuendesha matatu.
Kando na kuilaumu NTSA, wamiliki hao wa matatu pia walitupa lawama kwa wamiliki wa magari ya kibinafsi ambao wanafanya uchukuzi wa abiria chini ya maji.
“Hatuna njia ya mkato katika hili na ni wakati mwafaka kwa serikali kuwa makini na wale wanaomiliki magari ya kibinafsi lakini wamesababisha kutumia magari hayo kama matatu zinazopita njia mbalimbali. Hili ni kosa na linafaa kuangaliwa,” Bw Kimutai alisema.