Mwanaume mmoja ambaye alinusurika na shambulio la fisi miaka miwili iliyopita ameuliwa na ndovu katika Kaunti ya Machakos mashariki mwa Kenya, vimeripoti vyombo vya habari nchini humo.
Mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 72, Musili Musembi anasemekana kuwa alikanyagwa na ndovu alipokuwa akitembea kwenda nyumbani kwake Jumatano usiku.
Mizozo wa binadamu na wanyamapori ni ya kawaida katika maeneo yanayopakana na mbuga ya Wanyama ya Tsavo Mashariki , ambapo wakazi wamekuwa wakilalamika kushambuliwa na kuharibiwa kwa mimea yao na wanyamapori .
Mwaka 2020, marehemu Musembi alisemekana kupigana na fisi aliyekuwa ameshambulia mifugo wake, ambapo alipata majeraha kwenye mkono wake wa kushoto.
Alhamisi, wakazi wenye hasira walidai kufanya mkutano na waziri anayehusika na wanyamapori.
Pia walitaka Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya kumuondosha ndovu huyo.
Inasemekana polisi walifyatua risasi angani ili kuuchukua mwili wa Bw Musembi, ambao baadaye ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya mji wa Kibwezi.