Nitagombea urais 2026, mwanawe Museveni, Jenerali Muhoozi atangaza

Muhoozi alidai kuwa umefika wakati wa kizazi cha sasa kuongoza Uganda.

Muhtasari

• Muhoozi amedai kuwa amechoka kungoja kuwa Rais wa Uganda hivyo ana uhakika na kumrithi babake.

KWA HISANI
KWA HISANI
Image: Muhoozi Kainerugaba

Mwana wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Jenerali Muhoozi, ametangaza kuwa atagombea kiti cha urais katika  uchaguzi wa mwaka wa 2026 ili kumrithi babake.

Jenerali Muhoozi, kwa muda sasa amekuwa akizua hisia mseto na matamshi yake katika mitandao, alitoa tangazo hilo kupitia mtandao wa Twitter akisema kuwa watu wamekuwa wakimngoja sana atoe hilo tangazo hivyo aliweka wazi uwaniaji wake wa urais mwaka wa 2026.

"Mmetaka niiseme kwa muda mrefu ,sawa, kwa jina la Yesu Kristo Mungu wangu na kwa jina la watu wote wadogo wa  Uganda na dunia, na kwa jina la mapinduzi yetu nitagombea urais 2026!" alichapisha Jenerali Muhoozi.

Hapo awali Muhoozi alitangaza kuwa ana ari na uhakika ya kutaka kumrithi babake ambaye amekuwa rais wa Uganda tangu mwaka wa 1986 ikimfanya awe rais ambaye ameongoza kwa muda mrefu Afrika Mashariki.

Akionekana kumlenga babake ,Muhoozi alisema kuwa umefika wakati wa kizazi cha kisasa kung'aa kuliongoza taifa na kukoma kwa watu wazee kuwatawala

Muhoozi pia aliwasuta wale wanaojaribu kumzuia kutomrithi babake akisema kuwa wanapigana vita ambavyo hawawezi kushinda.

Muhoozi aliteuliwa na babake, Yoweri Museveni kuwa Jenerali wa Jeshi la Uganda. Muhoozi alidai kuwa Uganda inaweza kunyakua jiji la Nairobi kwa wiki mbili pekee,hata hivyo serikali ya Uganda ilijitenga na kauli yake ikisema kuwa hayo yalikuwa ni maneno yake Muhoozi na kuwa haongei kwa niaba Uganda.

Jenerali Muhoozi ana miaka 48 .Aliteuliwa kama mshauri wa rais mwaka wa 2017 ikazua shutuma kuwa alikuwa anatayarishwa kwa ajili ya urais.