Raila apuuzilia mbali uwezekano wa Ann Njeri kuwa mmiliki halali wa dizeli ya 17b

Odinga alisema kwamba kwa kumuangalia tu sura yake, Ann Njeri hakai mtu mwenye uwezo wa kuagiza mafuta ya gharama ya bilioni 17.

Muhtasari

• Huku akiingia kwenye mzozo huo, Raila alipuuzilia mbali msisitizo wa mfanyabiashara huyo kuwa shehena ya mafuta ni yake.

Raila Odinga
Raila Odinga
Image: Facebook

Kiongozi wa upinzani, Raila Odinga amekejeli uwezekano wa mfanyibiashara Ann Njeri kuwa mmiliki halali wa mafuta ta dizeli yenye utata ya shilingi bilioni 17 ambayo yameshikiliwa kwenye bandari ya Mombasa kwa Zaidi ya mwezi.

Njeri amekuwa katikati ya mzozo unaohusisha mafuta ya mabilioni ya mabilioni na kutoweka kwake kabla ya kupatikana salama siku kadhaa zilizopita.

Huku akiingia kwenye mzozo huo, Raila alipuuzilia mbali msisitizo wa mfanyabiashara huyo kuwa shehena ya mafuta ni yake.

Katika klipu moja ambayo imezungushwa kwenye mitandao ya kijamii, Odinga kwa mzaha alisema kwamba tajiri mwenye uwezo wa kuagiza shehena ya mafuta yenye thamani ya mabilioni ya pesa wala hana sura kama ya Ann Njeri anayeonekana mtu wa kawaida tu kutoka uchumi wa wastani.

"Sote tumemwona, na pia tunajua gharama ya kuagiza mafuta kutoka nje. Pesa ambazo zinatakikana ili ufanye biashara ya mafuta, Kwa kumtazama tu, unaweza kusema KSh 17 bilioni si zake. Angalia sura yake, Anawakilisha watu wengine ambao sasa tunataka kujua," Raila alisema huku akicheka.

Haya yanajiri wakati pia mamake Njeri akikiri kwamba wala hakuwahi kujua kama binti yake ana utajiri wa kiasi cha kumwezesha kuagiza mafuta ya gharama hiyo kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuuza kwenye soko la Kenya.

Akizungumza na runinga ya NTV, mamake alisema kwamba kwa muda wa miaka 5, hajaonana na mwanawe na wamekuwa tu wakifanya mawasiliano kwa njia ya video ya simu.