Dennis Itumbi adai serikali haiko nyuma ya kukamatwa na kushtakiwa kwa Nuru Okanga

"Najua kwa ukweli kwamba Rais William Ruto ana mambo mazito ya kufanya na HAPENDI drama kama hiyo na kukamatwa," Itumbi alisema.

Muhtasari

• Pia mwanablogu huyo alijitolea kumtaka wakili mmoja kuzungumza na Okanga ili kumwakilisha mahakamani iwapo atakubali.

Nuru Okanga na Dennis Itumbi
Nuru Okanga na Dennis Itumbi
Image: FaCEBOOK

Mwanablogu wa serikali ya Kenya Kwanza Dennis Itumbi ametoa taarifa ya kuashiria kwamba sio serikali ya rais Ruto ambayo iko nyuma ya kukamatwa kwa mtetezi mkali wa sera za Azimio la Umoja One Kenya, Nuru Okanga.

Itumbi kupitia ukurasa wake wa X aliandika kwamba hata wao kama serikali hawajui ni nani aliye nyuma ya kuhangaishwa kwa Okanga kisheria mara kwa mara.

Itumbi kama kawaida yake aliitetea serikali ya Ruto dhidi ya kukimbizana na Okanga akisema kwamba Bwana Ruto ana shughuli nyingi za maana ambazo anahitaji kuwafanyia Wakenya na wala si kumkamata mtu wa kawaida kama Okanga.

“SIKUBALI kabisa wazo la kuwakamata wanablog kwa kumtukana rais. Anayefanya hivyo wacheni kabisa. Najua kwa ukweli kwamba Rais @WilliamsRuto ana mambo mazito ya kufanya na HAPENDI drama kama hiyo na kukamatwa, hata hajui kuihusu. Kwa hiyo mlalamikaji ni nani hasa? Wachaneni na wanablogu, wajiexpress! Tafuteni kazi injini...” Itumbi aliandika.

Pia mwanablogu huyo alijitolea kumtaka wakili mmoja kuzungumza na Okanga ili kumwakilisha mahakamani iwapo atakubali, huku akisema yeye – Itumbi – atagharamia ada ya uwakilishi.

“Tafadhali wakili @W_Kinuthiah, ikiwa Nuru Okanga atakubali kumwakilisha mahakamani kwa gharama yangu. Kwa kweli kuna haki ya kuudhi, kushtua, au kuvuruga,” Itumbi alisema.

Hii inakuja saa chache baada ya Okanga kufikishwa mahakamani na kusomeshwa shtaka ambalo Wakenya wengi wanahisi waliomshtaki wanachukulia mambo kwa mzaha mno.

Katika hati hiyo ya mashtaka ambayo imewasilishwa mitandaoni, Okanga alifunguliwa mashtaka kwa kukejeli uongozi wa rais Ruto eti alimtaja kama mtu ambaye ni mjinga asiye na akili katika kuiongoza nchi.

Hii si mara ya kwanza kwa Okanga kuburuzana kisheria na kuishia mahakamani. Mapema Jumatano, aliandika katika ukurasa wake wa Facebook kwamba alitiwa mbaroni na makachero wa DCI bila kuambiwa sababu ya kukamatwa kwake.