Ufichuzi wa mkanda wa CCTV ulipelekea kukamatwa kwa wanaume wawili mjini Eldoret wanaohusishwa na mauaji ya mwanariadha wa Uganda Benjamin Kiplagat.
Kiplagat alipatikana ameuawa kwa kudungwa kisu kwenye gari mjini Eldoret usiku wa kuamkia mwaka mpya, polisi walisema Jumatatu.
Kisu kinachoshukiwa kutumika katika mauaji ya Kiplagat kilipatikana kwa mmoja wa washukiwa hao, kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Moiben Stephen Okal alisema.
Kiplagat alikuwa na umri wa miaka 34. Sababu ya mauaji hayo inaonekana kuwa wizi, alisema, kwa sababu pesa na simu ya rununu zilichukuliwa kutoka Kiplagat.
Koo la Kiplagat lilikatwa, polisi walisema. Alipatikana amekufa ndani ya gari la kakake mapema Jumapili viungani mwa Eldoret, mji wa mwinuko magharibi mwa Kenya unaojulikana kama kituo cha mazoezi ya wanariadha mashuhuri.
Kiplagat alishiriki katika michezo mitatu ya Olimpiki na ubingwa wa dunia sita katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi. Alishinda medali ya shaba katika michuano ya Afrika ya 2012.
Kiplagat ni mwanariadha wa nne kuuawa katika eneo hilo katika miaka ya hivi majuzi.
Bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za nyika Agnes Tirop aliuawa kwa kudungwa kisu nyumbani kwake katika mji wa karibu wa Iten mwaka wa 2021. Mumewe anakabiliwa na kesi ya mauaji.
Mwili wa mwanariadha wa Bahrain mzaliwa wa Kenya Damaris Muthee uliokuwa ukiharibika ulipatikana katika nyumba ya mwanariadha wa kiume wa Ethiopia mnamo 2022. Mwanariadha huyo ndiye mshukiwa mkuu wa kifo chake lakini bado hajakamatwa.
Mwanariadha wa Rwanda Rubayita Siragi aliuawa mwezi Agosti katika kile ambacho polisi wanaamini kuwa ni vita na mwanariadha mwingine kuhusu mwanamke.