logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanawe gavana Mwangaza miongoni mwa waliokamatwa kuhusiani na mauaji ya Sniper

Mwili wa mwanablogu huyo baadaye ulipatikana umetupwa katika Mto Mutonga.

image
na Davis Ojiambo

Habari06 January 2024 - 08:47

Muhtasari


  • • Juhudi za mke wa marehemu kuwasiliana naye hazikuzaa matunda na kumlazimu kuripoti polisi.
  • • Mwili wa mwanablogu huyo baadaye ulipatikana umetupwa katika Mto Mutonga.

Huku idara ya DCI ikiendelea na uchunguzi kubaini waliotekeleza mauaji ya kinyama ya mwanablogu wa kaunti ya Meru, Daniel Muthiani maarufu Sniper, Alhamisi watu wengine Zaidi walitiwa mbaroni.

Mwanawe wa kiume wa gavana wa Meru Kawira Mwangaza pamoja na nduguye gavana huyo ni miongoni mwa watu ambao walitiwa mbaroni na makachero wa DCI huku uchunguzi dhidi ya mauaji hayo ya kinyama ukizidi kushika kasi.

Kwa mujibu wa K24, wawili hao, Timothy Kinoti almaarufu Timo (mwanawe Mwangaza) na Murangiri Kenneth (kakake Mwangaza) walikuwa miongoni mwa washukiwa watano waliokamatwa Alhamisi, Januari 4, 2024, na kuzuiliwa katika vituo mbalimbali vya polisi jijini Nairobi na Kiambu.

Afisa wa DCI anayesimamia uchunguzi huo alithibitisha kwamba wawili hao ambao walikamatwa pamoja na Kenneth Mutua, Fredrick Muriuki, na Frankline Kimathi waliwasiliana na mwanablogu aliyeuawa, mkosoaji mkubwa wa Mwangaza, na kumwarifu kwamba atakutana na gavana huyo ili kurekebishana na kufanya kazi pamoja.

Kujibu mwito huo, mwanablogu huyo aliyeuawa alisafiri kutoka nyumbani kwake ndani ya Kaunti Ndogo ya Igembe Kusini hadi mjini Meru ambako alikutana na waliojibu na kutoweka baadaye.

Juhudi za mke wa marehemu kuwasiliana naye hazikuzaa matunda na kumlazimu kuripoti polisi.

Mwili wa mwanablogu huyo baadaye ulipatikana umetupwa katika Mto Mutonga.

"Hyrene Kawira Kamenchu, mke wa marehemu alijaribu kuwasiliana naye bila mafanikio na kumfanya atoe taarifa katika Kituo cha Polisi cha Maua," waraka huo ulisomeka kwa sehemu.

Afisa huyo pia alibainisha kuwa DCI bado haijawakamata washukiwa wengine waliohusika na mauaji ya mwanablogu huyo.

Idara ya upelelezi pia iliiomba Mahakama ya Kiambu kuruhusu maafisa wa upelelezi kuwazuilia washukiwa hao kwa siku 21 ili kutoa nafasi kwa uchunguzi.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved