Katibu wa kudumu wa elimu Belio Kipsang amefichua mipango ya serikali ya kuanzisha ushuru mpya kwa baadhi ya bidhaa za vyakula vinavyoagizwa kutoka nje kufadhili mpango wa kulisha wanafunzi shuleni.
Akiwa mbele ya kamati ya kitaifa ya kitengo cha elimu mnamo Jumanne, Juni 11, Kipsang alifichua kuwa wizara ilikuwa katika harakati na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya (KRA) kuhusu uwezekano wa kutoza kodi kwa vyakula vilivyotoka nje.
Vilevile, alieleza kuwa, kupitishwa kwa tozo hizo ni mojawapo ya mikakati inayolenga kufadhili mpango huo uliokuwa ukikumbwa na masaibu ya kifedha.
"Kulikuwa na mpango wa kushinikiza asilimia 2.5 ya mapato ya nchi kuelekea kwa mpango huo," alinena.
Aliendelea kufichua kuwa, "wizara ilikuwa katika mazungumzo na Mamlaka ya Ushuru ya Kenya ili kutoza ushuru kwa vyakula visivyofaa vinavyoagizwa kutoka nje ili kuangazia mpango wa kitaifa wa ulishaji," ilisoma taarifa kutoka Bunge.
Hata hivyo, maelezo zaidi kama vile kiwango cha ushuru na tarehe inayowezekana ya kuanza kwa ushuru huo haikufichuliwa.
Baadhi ya vyakula visivyofaa vinavyotumiwa na wakenya ni pamoja na keki. , biskuti, chokoleti, peremende, nyama iliyosindikwa kama vile Bacon na vinywaji vya sukari miongoni mwa vingine.
Kwa hiyo, pamoja na kutozwa ushuru, bei ya vyakula itapanda maradufu kuliko awali.
PS Kipsang hata hivyo aliwahakikishia wanachama kwamba licha ya changamoto zilizopo, kama mwanachama wa Global School Meals Coalition, Kenya ilijitolea azma ya kufikia ulishaji wa shule kwa wote ifikapo 2030 kwa kuongeza kiwango cha sasa cha huduma kutoka kwa wanafunzi milioni 2.6 hadi milioni 10.
Kwa mujibu wa PS, mpango huo umeongezeka taratibu na kufikia jumla ya wanafunzi milioni 2.6 katika shule 8,185 kote nchini kufikia 2024.