Mwakilishi wadi ya Kileleshwa kaunti ya Nairobi, Robert Alai ametoa rai kwa waandamanaji jijini Nairobi kusitisha maandamano yao.
Kupitia ukurasa wake wa X, Alai akiwaomba vijana hao kusitisha mpango wao wa kupeleka maandamano hayo katika ikulu ya rais Ruto akisema kwamba tayari takwa lao kuu la kutupilia mbali mswada wa fedha tayari limetekelezwa na rais.
MCA huyo wa ODM alisema kwamba sasa vijana wa Gen Z hawana kisingizio kingine cha kuendeleza maandamano yao kwani rais ameshafanya jinsi walivyokuwa wanashikiniza.
Alisema mtu yeyote ambaye anashinikiza kuendelea na maandamano sasa analenga kupata tope uhalali wa shinikizo lao kwa rais ambalo lilidumu kwa takribani wiki mbili.
“Nani sasa anahamasisha vijana kwa maandamano zaidi anaua uhalali wao na kuwaharibia kwamba hawatachukuliwa uzito tena. Msiende kwa STATE HOUSE. Ikiwezekana, msiandamane leo,” Alai alirai.
Vijana wa Gen Z kwa wiki mbili sasa wamekuwa wakishinikiza kuondolewa kwa mswada tata wa fedha 2024 katika jukwaa la X wakitumia alama ya reli #RejectFinanceBill2024.
Hata baada ya wabunge wengi kuupigia kura mswada huo kuupitisha, rais hapo jana katika hotuba yake akidinda kuutia saini na kuwa sheria, akisema kuwa amesalimu amri kwa shinikizo la Wakenya.