Wanyama awataka polisi kukomesha mauaji wakati wa maandamano

Kiungo huyo wa CF Montreal alisikitishwa na mauaji ya raia ambao alisema kuwa walikuwa wanapigania haki yao huku akitaka haki itendeke.

Muhtasari

•Wanyama amewaomba polisi kutotumia nguvu nyingi wakati wa kukawakabili waandamanaji hii ni baada ya maandamano kuhusu mswada wa fedha 2024.

Image: INSTAGRAM// VICTOR WANYAMA

Nahodha wa zamani wa Harambee Stars, Victor Wanyama ameeleza kutoridhishwa kwake na hatua kali za vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya hivi majuzi ya kupinga mswada wa fedha nchini Kenya.

Olunga alisema haya kufuatia kipindi cha msukosuko kilichobainishwa na machafuko ya umma dhidi ya mapendekezo ya nyongeza ya ushuru harakati ambayo ilifikia kilele kwa uamuzi wa serikali wa kubatilisha mswada wa fedha ,2024

Wanyama, ambaye kwa sasa anacheza kama kiungo wa CF Montreal, alitumia ukurasa wake wa Instagram kueleza kusikitishwa kwake na mshikamano wake na waathiriwa wa mapigano hayo makali.

"Demokrasia ni serikali ya watu. Na watu,kwa watu. Moyo wangu unawaendea watu wasio na hatia waliopotea wakati wa maandamano. Kila mtu ana haki ya kusikilizwa. Heshimu maisha," Wanyama alisema.

 Wanyama pia alilalamikia hali iliyosababisha hatua hizo kali za waandamanaji hao, akisema, "Mashujaa wetu, walistahili bora," huku akitaka haki itendeke kwa walioangamia.

Mswada wa fedha ulioondolewa wa 2024 ulianzishwa awali kama hatua ya kushughulikia deni kubwa la Kenya, ambalo linazidi dola bilioni 80.

Serikali ilisema kuwa bila kuongezeka kwa mapato ya kodi, ambayo kwa sasa nusu yake yanatumiwa na ulipaji wa deni, uthabiti wa uchumi wa nchi unaweza kuzorota zaidi.

Hata hivyo, mapendekezo ya nyongeza ya kodi yalionekana na wengi kama mzigo mzito, hasa wakati wa kuimarika kwa uchumi na ugumu wa kifedha ulioenea.

Hata hivyo serikali, hatimaye ilikubali shinikizo la umma. Rais alisema hatatia saini mswada huo kuwa sheria katika tangazo lililokuja siku chache kabla ya ghasia mbaya zaidi kuzuka.