KMPDU yakanusha madai ya kuuawa kwa daktari kwenye maandamano

Wamekana kwani aliyepigwa na kitoa machozi alikuwa mnunuzi wa dawa kwenye kemia

Muhtasari

•Mwanamke anayeitwa Margaret Obuya alitambuliwa kimakosa kuwa daktari alipokuwa kwenye harakati za kununua dawa katika kemia ya Transchem 

•“Tumewasiliana na Bi Margaret Obuya ambaye alitambulika kimakosa kuwa daktari. Alipigwa na kitoa machozi alipokuwa akinunua dawa katika duka la Transchem Chemist CBD wakati wa maandamano.

Dr Davji Bhimji Attelah
DKT. Davji Bhimji Attelah Dr Davji Bhimji Attelah
Image: FACEBOOK//Dr Davji Bhimji Attelah

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU) Jumanne ulipuuza  uvumi kwamba daktari mmoja alikuwa miongoni mwa waliouawa wakati wa maandamano ya kupinga serikali. 

Wiki iliyopita, ripoti za mitandao ya kijamii zilidai kuwa daktari mmoja wa kike alipigwa risasi na maafisa wa polisi na kutangazwa kuwa amefariki alipofika hospitalini. 

Katibu Mkuu wa KMPDU Davji Atellah, hata hivyo, alifafanua kuwa mwanamke anayeitwa Margaret Obuya alitambuliwa kimakosa kuwa daktari alipokuwa kwenye harakati za kununua dawa katika kemia ya Transchem eneo la CBD wakati wa maandamano. 

Mwanamke huyo alifichua kuwa alipigwa na kitoa machozi na baadaye kulazwa kwa matibabu ya dharura katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) kutokana na majeraha yake.

Atellah alithibitisha kuwa ameruhusiwa kutoka hospitalini na anazidi kupata nafuu nyumbani. 

“Tumewasiliana na Bi Margaret Obuya ambaye alitambulika kimakosa kuwa daktari. Alipigwa na kitoa machozi alipokuwa akinunua dawa katika duka la Transchem Chemist CBD wakati wa maandamano.

Alilazwa kwa matibabu ya dharura katika hospitali ya Kenyatta kwa ajili ya majeraha yake, Margret ameruhusiwa na kwa sasa anaendelea kupata nafuu nyumbani,” taarifa hiyo ilisomeka kwa sehemu.

"Kama Muungano, tunaendelea kulaani matumizi haramu ya nguvu zisizo na uwiano zinazofanywa na maafisa wa usalama dhidi ya waandamanaji wasio na silaha, wakiwemo madaktari, wanasheria na waandishi wa habari.

Tunaitaka IPOA kuwachunguza na kuwashtaki maafisa wote wanaopatikana na hatia. Wananchi wana uhuru wa kikatiba wa kuandamana. Haki na lazima zilindwe." Alimalizia.