Mvua itanyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi wiki hii, kuashiria kilele cha msimu wa baridi zaidi nchini Kenya.
Hali ya hewa ya baridi ya Juni-Agosti kawaida hufikia kilele mnamo Julai, ingawa halijoto itasalia kuwa joto kuliko kawaida mwezi huu. Mtaalamu wa hali ya hewa alisema maeneo mengi ya nchi yatapata hali ya baridi na mawingu ya mara kwa mara, lakini baadhi yatakuwa na mvua.
“Mvua inatarajiwa kunyesha katika baadhi ya maeneo ya nyanda za juu mashariki na magharibi mwa bonde la ufa, bonde la ziwa Victoria, bonde la ufa, Pwani na kaskazini-magharibi mwa Kenya..." Dkt Kennedy Thiong’o, naibu mkurugenzi wa idara ya hali ya hewa ya Kenya alisema.
Alisema kaunti mbalimbali zinatarajiwa kuwa na mvua mwishoni mwa juma hili. Hizi ni Kaunti za Kisii, Nyamira, Nandi, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Siaya, Kisumu, Homabay, Busia, Migori, Narok, Baringo, Nakuru, Trans-Nzoia, Uasin-Gishu, Elgeyo-Marakwet na Pokot Magharibi.
"Vipindi vya jua vinatarajiwa asubuhi ingawa maeneo machache yanaweza kupata mvua katika nusu ya pili ya kipindi cha utabiri. Mvua ya alasiri na usiku na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache mara kwa mara na kuenea katika maeneo kadhaa,” Thiong’o alisema, kuhusu kaunti hizi.
Kaunti za Turkana na Samburu pia huenda zikawa na mvua za asubuhi na manyunyu ya alasiri/usiku na mvua za radi zinatarajiwa katika maeneo machache katika nusu ya pili ya kipindi cha utabiri.
Katika Kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang'a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka-Nithi na Nairobi, huenda asubuhi kukawa na mawingu huku mvua ndogo ikinyesha sehemu chache, hivyo kutoa mwanya kwa vipindi vya jua.
Sehemu nyingine ya nchi itakuwa na hali ya mawingu mara kwa mara ambayo inatarajiwa kutoa nafasi kwa vipindi vya jua. Usiku kuna uwezekano wa kuwa na mawingu kiasi.